Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Maftaha Abdallah Nachuma

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtwara Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, suala la utawala bora ni pamoja na Serikali kushirikisha wananchi. Nchi hii ina mfumo wa ushiriki wa wananchi kupitia wawakilishi wanaochaguliwa na wananchi wenyewe. Wawakilishi hao ni Wenyeviti wa Mitaa, Madiwani, Wabunge pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano na Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kushangaza sana kumekuwepo na mpango wa makusudi wa kuzuia wawakilishi kufikisha kero za wananchi pale viongozi wa Kitaifa wanapotembelea maeneo yetu, kwa mfano Mtwara Mjini, Novemba 6 mwaka jana, mwaka 2018, tulizindua Mji Mkongwe wa Mikindani ambapo mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Hasunga, lakini jambo la kushangaza Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara alikataa mimi Mbunge wa Jimbo kusalimia wananchi katika mkutano nilioshiriki kwa kiasi kikubwa kuwaomba wana Mtwara Mjini kushiriki uzinduzi huo, hali iliyosababisha wananchi wengi kuchukia sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilipomuuliza Mkuu wa Mkoa kwa nini hanipi nafasi, alisema kwa mdomo wake kuwa, hivyo ndivyo tulivyopanga kama hujaridhika fanya unavyojua wewe. Kama Mbunge niliumia na kauli ya Mkuu wa Mkoa kwani alitaka mimi nibishane naye ili apate kick ya cheo chake. Niliamua kukaa kimya nikafikisha kwenye kikao na Mheshimiwa Waziri akasema kweli haikuwa sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 2 Aprili, 2019 Mheshimiwa Rais alikuja Mtwara Mjini kufungua miradi kadhaa, siku mbili kabla tulipewa ratiba ya ziara hiyo. Tukiwa kwenye uwanja wa mkutano, Airport Mtwara, nilimuuliza Mkuu wa Mkoa kuhusu utaratibu wa Mbunge wa Jimbo ambaye ni mwenyeji kuhusu ukaaji, kusalimia na kumpokea Mheshimiwa Rais pale aliposhuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasikitika kusema kuwa, Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya na baadhi ya Wabunge wa chama tawala walikataa mimi Mbunge mwenyeji:-

(a) Walinizuia kwenda kumpokea Mheshimiwa Rais badala yake wakawekwa watu wa CCM na yeye mwenyewe Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya tu wakati mimi ni Mbunge mwenyeji;

(b) Mkuu wa Mkoa wa Mtwara akanizuia hata kukaa viti vya nyuma ya Rais, kama Mbunge mwenyeji, wakasema huruhusiwi kukaa huku hata kama ni Mbunge, viongozi wa CCM wamepewa nafasi; na

(c) Mkuu wa Mkoa akanizuia hata kusalimia wananchi wangu na kumkaribisha Mheshimiwa Rais, kama Mbunge mwenyeji. Mbaya zaidi nilipouliza kwa nini mnamzuia Mbunge aliyechaguliwa na wananchi wengi, wakaniambia ungekuwa CCM ungepewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunaomba kujua utawala bora tunaozungumza ni wa aina gani? Kwani huyu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara na DC wa Wilaya ya Mtwara hawajui kama nchi hii ni ya vyama vingi na Mbunge wa Jimbo ni kiongozi halali kikatiba? Naomba kujua kwa nini umlazimishe mtu kuhama chama?

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini nimeamua kufanya siasa safi kwa kuwa, nataka amani na utulivu Mtwara Mjini na Kusini kwa ujumla. Haya yanayofanywa na Mkuu wa Mkoa na DC kwa utashi wake noamba yakomeshwe mara moja maana nguvu ya Mbunge wa Mtwara Mjini kwa wananchi ni kubwa sana, nddio maana nikifanya mikutano Wananchi wananiitika sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata kama humuhitaji Mbunge wa CUF, lakini ndio kawekwa na wananchi wa Mtwara Mjini, lazima apewe heshima na haki yake kama mimi ninavyowaheshimu RC, DC na Wabunge wote wa CCM nawaheshimu sana. Naomba tuendelee kutunza heshima hii na amani ya Mtwara kwa kuheshimiana, kama wote viongozi wa wananchi.