Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Mwantum Dau Haji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. MWANTUM DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa ruhusa yako nami napenda kuongelea katika taarifa hizi mbili za Wizara ya TAMISEMI na Serikali za Mitaa. Kwanza niweze kumpongeza Waziri wangu Mheshimiwa Jafo pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuchika.

Vilevile niwapongeze na Manaibu wake wote aliokuwa nao jinsi wanavyoweza kufanya kazi. Pia nampongeza mama yangu Mary Mwanjwela kwa kuteuliwa kuwa Naibu wangu wa TAMISEMI na Serikali za Mitaa. (Makofi)

MWENYEKITI: Hebu jina likae, vizuri Mheshimiwa Mwantumu. Mheshimiwa Mwanjelwa.

MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwanjelwa nakupongeza sana, kuwa Naibu wangu wa Utawala Bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende moja kwa moja kwenye mchango wangu, kwanza nianze kuzungumzia suala la TARURA. TARURA ni chombo ambacho kinafanya kazi vizuri na wanafanya kazi kwa juhudi kubwa, lakini kila anayesimama hapa anaisifu TARURA. Katika kutembelea miradi yetu, nimeiona TARURA kama kweli inafanya kazi tulipokwenda Mtwara na nimeziona barabara zile za TARURA jinsi zinazofanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichokiona pale juu ya zile barabara, kuna barabara zimejengwa 2017 tu, lakini tayari zimeshaanza mashimo. Katika kuangalia barabara zile, mimi nahisi yale malori yetu ambayo yanasimama katika barabara, yanamwaga oil. Zikishamwaga oil, zile barabara zinavimba, zinafanya mashimo halafu utaziona zipo kwenye uchakavu, kumbe zile barabara bado zingali mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuogelea katika suala hili napenda Serikali ifanye juu chini kutokana na zile barabara za TARURA na yale malori jinsi yanavyomwaga ile oil waweze kuzifuatilia na kuzifanyia utaratibu kamili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niogelee katika suala la mradi wa TASAF. Kila ninaposimama nazungumzia mradi wa TASAF, nawapongeza sana kwa sababu wanafanya kazi nzuri na kila siku nikisimama huwa nawaambia big up, maana wanafanya kazi kwa hali na mali, watu wetu ambao waliokuwa wanyonge hivi sasa hivi wana wanajisikia kutokana na TASAF inavyofanya kazi. Wale watu wanapata pesa za TASAF, kisha wanafanya miradi yao na ile miradi yao inaonekana; kuna wengine wana ufugaji wa mbuzi, kuna wengine wanajenga nyumba zao, wanapata kustirika na wengine wanapeleka watoto wao shuleni. Kwa hiyo, naomba sana, TASAF isije ikaondolewa maana tayari ni mkombozi wa wanyonge katika Tanzania yetu hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niogelee pia kwenye suala la uzazi salama; hivi sasa hili neno lazima tuliweke mbele kutokana na watoto wetu. Uzazi salama, watoto wanapokuwa wamezaliwa na wazazi wao tayari wanakuwa wanashughulikiwa na watoto wale kila mmoja anapata haki yake kwa mama yake. Hata hivyo, kuna suala nimeliona kwa macho yangu Dar es Salaam, kuna watoto ambao wanapelekeshwa na wazazi wao, wanakaa pembeni ya barabara na wanatumwa watoto wa miaka minne waje pale kwenye barabara zile, gari zinapokuwa zimepaki, kuja kuomba pesa. Hapa tayari wale watoto wameshakuwa wanaanza kudhalilika, maana wazazi wamekaa pembeni watoto wao ndio wanaotumikishwa. Kwa hiyo, naiomba Serikali ifanye juhudi juu chini, juu ya kazi zao wanazozifanya, maana inaonekana limepungua sana suala lile la ombaomba na kuwatumikisha watoto, lakini bado hili suala linaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niogelee katika suala la Bodi ya Mishahara ya Watumishi wa Umma. Bodi hii nimeangalia hapa vizuri tu katika taarifa ya Mheshimiwa Mkuchika kwamba kuna watumishi wa umma ambao wanafanyiwa utaratibu wa mishahara yao wapate kulipwa maslahi yao kiuhakika. Hata hivyo, bado watumishi wa umma wanasikitika hawapati mishahara yao kikamilifu na bado wanasikitika hawajaongezewa mishahara. Mishahara yao bado haijaongezwa na bado inakawia kuingizwa ili wajikwamue kimaisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mchango wangu kwa hii leo nilikuwa nataka nijikite katika masuala hayo. Pia nataka kumpongeza Rais wangu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa jitihada zake anazozichukua hivi sasa kuzungukia mikoa yote na kesho tukijaaliwa tunaambiwa yuko hapa Dodoma. Kwa hiyo, nampongeza sana pamoja na Makamu wake, wanafanya kazi vizuri, waendelee kufanya kazi ili wazidi kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)