Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kupata nafasi hii kuchangia kwenye Wizara hizi mbili ambazo ni muhimu sana; Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Utumishi na Utawala Bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nawasifu sana Mawaziri wote wawili kwa kazi nzuri ambazo wanazifanya. Namsifu sana Mheshimiwa Mkuchika na Naibu wake Mheshimiwa Mary kwa kweli tangu amehamishiwa kwenye wizara hiyo, wizara imetulia. Pia ningependa kuvisifu vyombo vya ulinzi na usalama kwa sababu kazi ambazo wanazifanya sasa hivi za usalama sio siri kwamba uko vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongezakwa dhati kabisa kazi zinazofanywa na Mheshimiwa Rais na napongeza kabisa kazi ambazo wanafanya Mawaziri wa TAMISEMI hasa Mheshimiwa Jafo, Mheshimiwa Kandege na Mheshimiwa Mwita Waitara. Kwa kweli kazi ni nzuri na kwa kweli wanastahili sifa kubwa sana. Wamezunguka sana kwenye hii nchi na wamezunguka sana hasa kwenye Wilaya yetu; nakumbuka Mawaziri wote hao ninaowataja wamefika Muheza na wameona kazi za Muheza ambazo wanazifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Muheza tumefaidika sana kwa sababu tumepewa kwanza bilioni 1.5 kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya na kwenye mpango wa mwaka huu pia tumeongezewa milioni 500 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya. Pia tulipewa karibu milioni 400 kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Mkuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunajenga vituo vya afya kwenye kila Tarafa; kwenye Tarafa ya Amani, Misarai tunajenga kituo cha afya, Tarafa ya Bwembera tunajenga Potwe na Mhamba na kwenye Tarafa ya Ngomeni tunajenga Umba. Nakumbuka nilikuja ofisini na Mheshimiwa Waziri aliniahidi katika vituo vyote hivyo atajitahidi kadiri anavyoweza kuhakikisha kwamba kituo kimoja ananipa milioni 400 kwa ajili ya jiografia ya Jimbo lenyewe kwa sababu ya ukubwa wa Jimbo lile. Hata hivyo, nimeangalia kwenye kitabu bahati mbaya sijaona kituo chochote ambacho kimepangiwa wakati huu, lakini namwomba Mheshimiwa Waziri ajaribu kufikiria kutokana na ukubwa wa Jimbo la Muheza ambalo ni kubwa sana lenye kata karibu 37 na vijiji karibu 135.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la maboma na madarasa, tunashukuru sana Muheza tumepata milioni 225 kwa ajili ya kukamilisha maboma ya shule za sekondari na tumeweza kuanza kazi hiyo karibu kwenye sekondari tisa. Kazi hiyo inaendelea vizuri, isipokuwa tunalo tatizo kubwa sana ambalo ni la maabara, tuna maabara karibu shule zote za sekondari, karibu sekondari 21. Haya ni maboma ya maabara ambayo tulitegemea kabisa Serikali itusaidie kukamilisha maabara haya, hii imeleteleza tatizo linafanya hasa wanafunzi wa sekondari katika Wilaya ya Muheza kutokusoma sana masomo ya sayansi. Kwa hiyo, tunawashukuru sana na tunaomba sana kwa msisitizo mkubwa kwamba tuletewe fedha nyingine za maboma ya maabara ili tuweze kumaliza hili tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la upungufu wa watumishi pamoja na Walimu; suala hili ni kubwa sana na nitamwandikia barua Mheshimiwa Waziri kumpa takwimu sahihi ambazo zinaonesha upungufu ulivyo mkubwa hasa kwenye masomo ya sayansi na hisabati. Tuna upungufu mkubwa na upungufu hasa wa Wauguzi pia na Madaktari kwenye zahanati na hiki kituo chetu cha afya ambacho tunategemea kukifungua karibuni. Kwa hiyo, tunategemea kwamba upungufu huu utaweza kukamilika na kuweza kusaidiwa kuweza kupata Walimu hasa wa sayansi na hisabati kwenye sekondari.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna upungufu mkubwa pia kwenye shule za msingi. Shule nyingi za msingi zina Walimu kuanzia wawili, watatu, wanne; huwezi kutegemea Walimu wachache na shule ziweze kufanya vizuri. Matokeo yetu ya mitihani ya shule za sekondari na msingi sio mazuri kutokana na kuwa na Walimu wachache. Kwa hiyo, nashukuru kwamba tuweze kuangaliwa na kupewa Walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala ambalo wenzangu wameliongelea la Madiwani, Madiwani tunawategemea sana kwenye hii miradi ambayo inaendelea sasa hivi. Wanafanya kazi kubwa sana Madiwani kwa sababu hasa Force Accountkwenye vituo vya afya na madarasa wanajituma sana na wanakuwa ni wahamasishaji wakubwa sana kwa wananchi wetu, ni vizuri suala lao la posho likaangaliwa ili waweze kuongezewa posho waweze kupata posho ambazo ni nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la TARURA, wenzangu wameolingelea kwa wingi sana lakini fedha ambazo wanapewa TARURA kutokana na kazi yao kubwa ni ndogo sana. Ni afadhali sasa hivi badala ya ile 70kwa30 basi ikaongezeka kidogo. Sisi kwenye Kamati ya Baajeti tunajitahidi kwa kadiri ya uwezo wetu kuhakikisha kwamba kwa kweli pendekezo hili linaweza kuchukuliwa kwa sababu TARURA kazi wanazofanya ni kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la miradi ya mikakati; miradi ya mikakati sisi Muheza tunategemea kujenga stendi ya kisasa na tumeleta maombi yetu yote na tunaamini yametelekezwa kwa ukamilifu kabisa, lakini tumeangalia pia hapa sikuona Muheza ikipewa chochote. Nilikuwa nafikiria Waheshimiwa Mawaziri wajaribu kwa kadiri ya uwezo waowaangalie kwamba wanaweza kutusaidia vipi, tunaamini kabisa kwamba tutakapopata fedha hizo za kujenga stendi mpya pale Muheza, basi tutaweza kujikimu na kuweza kujishughulikia na mambo yote ambayo tunayaweza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana na naunga hoja mkono. (Makofi)