Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi kuweza kuchangia Wizara hii ya TAMISEMI na Utawala Bora. Kwanza napenda kutumia nafasi hii kuipongeza Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa ambazo inafanya, ama miradi mikubwa ambayo inatekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona miradi kama Stieglers Gorge ambapo kwa ukamilishaji wa mradi huu tutapata Megawati kama 2,100 za umeme, tunaona ujenzi wa Standard Gauge (SGR), ujenzi wa kisasa wa reli yetu, tunaona usambazaji wa umeme vijijini, vijiji vyote vitapata umeme, tunaona vituo vya afya na hospitali karibu 67 zinajengwa nchi nzima. Miradi hii yote ikikamilika, ninaamini Tanzania itakuwa kati ya nchi 10 bora katika Bara la Afrika out of 54 countries. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo za Serikali katika kutekeleza miradi mikubwa, binafsi naunga mkono na wananchi wa Jimbo la Manonga wanaunga mkono harakati zote za Mheshimiwa Rais kupeleka nchi yetu katika uchumi wa kati. Sasa nianze kwa maombi yangu kama Wilaya na Jimbo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ya TAMISEMI, kwanza nawashukuru kwa kunipatia fedha kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Simbo. Kituo kimekamilika, sasa kilichobaki ni vifaa tiba. Naiomba Wizara ya TAMISEMI ituletee vifaa tiba katika Kituo chetu cha Afya cha Simbo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine nawaomba Wizara ya TAMISEMI, Jimbo letu ni kubwa sana. Mwaka 2018 Agosti, alikuja Mheshimiwa Waziri Mkuu Jimboni, alituahidi kutupatia fedha shilingi milioni 400 kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Choma cha Nkola.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya cha Choma baada ya Hospitali ya Wilaya ya Igunga kinachofuatia ni Kituo cha Afya cha Choma ambacho kinafanya operation ndogo ndogo. Karibu operation 150 wamekwishafanya, lakini changamoto iliyoko pale hatuna jengo la akina mama na watoto, hatuna jengo la kufulia nguo, hatuna mortuary, hatuna ward ya akina baba. Kwa hiyo, bado operation hizi wanapata changamoto sehemu ya kuwahifadhi wagonjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, nimeangalia kitabu chake sijaona bajeti ya fedha ambazo Mheshimiwa Waziri Mkuu aliahidi katika ziara yake. Tunaomba fedha kwa ajili ya ujenzi na upanuzi wa Kituo cha Afya cha Choma cha Nkola ili kuweza kuhakikisha kwamba tunasogeza huduma bora kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona bajeti hapa ya Wizara ya Afya. Tumetenga fedha za ujenzi wa hospitali katika Wilaya mbalimbali nchini. Wilaya yetu ya Igunga Makao Makuu ya Wilaya ni Igunga. Pale tuna hospitali ya wilaya. Hospitali yetu imechakaa sana, hatujapata fedha za maboresho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri tuangalie katika Hospitali ya Wilaya ya Igunga, hatuna ambulance. Nilinunua ambulance nikapeleka kwenye Kituo changu cha Afya cha Simbo. Sasa inachukuliwa ile ambulance ya kijijini, kwenye Kituo cha Afya cha Simbo, inaletwa mjini. Kwa hiyo, ile adha ambayo nilikuwa nimeenda kupunguza kwa wananchi inakosekana. Tunaomba ambulance ya wilaya iletwe, ili iweze kuhudumia kwa sababu mahitaji ni makubwa na katika makao makuu ya wilaya watu ni wengi sana wanahitaji kupata huduma hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tena tupate fedha kwa ajili ya kuongeza matengenezo kwani hospitali ya wilaya imechakaa, haina uzio, hakuna maabara ya kisasa. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri kwa sababu, mpo hapo Wizara ya TAMISEMI, mtupatie fedha kwa ajili ya kuboresha hospitali yetu ya wilaya ili kuboresha na kusaidia kupatikana huduma za afya katika Wilaya yetu ya Igunga, hasa Makao Makuu ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie kwenye shule za Serikali za wasichana. Tumeona ujenzi wa shule za Serikali za wasichana zikijengwa maeneo mbalimbali katika nchi yetu. Tabora Mjini tunayo natambua iko Tabora Girls, nimeona Nzega pale imejengwa. Naomba sasa, katika Wilaya yetu ya Igunga hatuna shule hata moja. Mimi binafsi katika Jimbo langu niko tayari na tuko tayari kutoa kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa shule, tukishirikiana na TAMISEMI, tutajenga pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba shule hizo za wasichana zijengwe katika Wilaya yetu ya Igunga pale Choma cha Nkola iweze kusaidia watoto wa kike wanaotembea umbali mrefu kutoka vijijini, kilometa nyingi kuja shuleni. Kwa hiyo, tukijenga shule hii itasogeza huduma, lakini itawarahisishia watoto hawa wa kike kukaa shuleni na kusoma kwa utulivu, itasaidia kuongeza ufaulu wao katika maisha yao ya kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiachilia mbali hilo, niiombe TAMISEMI, tuna upungufu wa ma-engineer. Engineer (mhandisi) wetu wa Wilaya tuliyenaye kwa masuala ya majengo inawezekana uwezo wake ni mdogo. Naomba TAMISEMI mtuletee engineer ambaye ataweza kutusaidia kuweza kusukuma hizi kazi za Kiserikali ambazo mmetuletea fedha ziweze kwenda kwa usahihi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia engineer wetu, tunanunua vifaa vingi sana mwisho wa siku vinabaki store, halafu inakuwa ni hasara katika maeneo yetu. Mfano ni Kituo cha Afya cha Simbo, tumenunua vifaa vingi hali ambayo imesababisha hata fedha tuliyonayo tumeshindwa kuwalipa wakandarasi wanaotudai. Naomba TAMISEMI ituletee engineer ambaye ataweza kwenda na hesabu ambazo zitaweza kukidhi mahitaji sambamba na maeneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia katika upande wa TARURA. Upande wa TARURA fedha inayopata katika Mkoa wa Tabora ni ndogo sana. Mkoa wa Tabora ni mkubwa kijiografia, ni mkoa wenye square metre karibu 75,000, miundombinu yake ya barabara ni mikubwa sana, lakini fedha inazopata ni ndogo, hazilingani na mahitaji ya mkoa wenyewe. Naomba TAMISEMI iangalie kutuongezea fedha katika upande wa TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna ujenzi mkubwa sana wa madaraja. Kwa mfano Mkoa wa Tabora kuunganisha na Shinyanga. Kila sehemu kuna madaraja, kuna Mto mkubwa wa Manonga. Kwa hiyo, ili uweze kuvuka upande wa pili inabidi kuwe na daraja. Kwa hiyo, mahitaji ya madaraja ni mengi sana katika maeneo yetu, lakini fedha tunazoletewa ni ndogo, haziwezi kukidhi mahitaji ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba TAMISEMI ituongezee fedha upande wa TARURA tuweze kujenga daraja la Mto Manonga upande wa Mondo ili kurahisisha wananchi wetu kuweza kwenda Shinyanga kwa urahisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia suala la utawala bora, kuna watumishi wengi sana wamekaa katika Halmashauri ya Wilaya ya Igunga wanakaimu miaka mitatu, miaka minne, wakati tuna uwezo wa kuwapitishia hizo nafasi wakaweza kuzimiliki, wanalipwa fedha za kukaimu muda mrefu. Ni hasara kwa Serikali na Taifa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Gulamali. Thank you. (Makofi)

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)