Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Allan Joseph Kiula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kwenye hoja iliyo mbele yetu. Kwanza kabisa, niseme mwanzo kabisa naunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuunga mkono hoja, napenda niseme maneno machache ya utangulizi. Cha kwanza tunatoa pongezi kubwa kwa Serikali ya Awamu ya Tano ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa inayofanya. Sote tumeshuhudia Waziri Mkuu ametembea karibu mikoa yote Tanzania akifanya kazi kubwa za kuleta maendeleo ikiwepo kuhamasisha shughuli za maendeleo na usimamizi mzuri wa fedha za umma na hiyo imeleta ari kubwa kwa wananchi kuona kwamba Serikali yao inafanya kazi nzuri na kazi iliyotukuka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna msemo unaosema Roma haikujengwa kwa siku moja, sasa watani zetu kila wakisimama hapa wanasema jambo hili halijafanyika, tunakwenda polepole lakini katika miaka hii minne sote tumeshuhudia kazi kubwa ambayo imefanyika. Hivi tunavyozungumza Rais alikuwa Kanda zile za Kusini alikuwa anafanya kazi kubwa ya kuhamasisha maendeleo na kufungua miradi mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, ziko kazi kubwa zimefanyika ambazo zimeshazungumzwa na kwenye kitabu zimeandikwa kwa hiyo sina sababu ya kuzirudia lakini Watanzania wote wanaona kazi hizo. Napenda kuzungumza jambo moja kwa msisitizo sana nalo ni kilimo kwa ujumla wake. Watanzania wengi zaidi ya asilimia 70 wanategemea kilimo, sasa tunapozungumza kwenda kwenye uchumi wa kati na chenyewe kinatakiwa kibadilike, tupate ukombozi wa kilimo. Ili tupate ukombozi wa kilimo tunaelewa uchumi wa Watanzania, tunao wakulima wadogo wadogo wanalima kwa jembe la mkono na sehemu zingine wanalima kwa kutumia ng’ombe, kwa hiyo, hawawezi kujikombo katika suala zima la kilimo.

Mheshimiwa Spika, kwenye hotuba limezungumzwa suala la kuimarisha Benki yetu ya Maendeleo ya Kilimo. Napenda kushauri kwamba benki hiyo iimarishwe na tuione vijijini kwa sababu unakuta benki hizi zinanufaisha baadhi ya watu wa mijini ambao pia siyo wakulima. Kwa hiyo, benki hii ikifika vijijini tutaweza kuwasaidia wakulima wetu.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni suala zima la mazao ya kimkakati. Tumeona Waziri Mkuu ameweka juhudi kubwa kuhimiza kilimo cha pamba, korosho lakini pia alikwenda Kigoma kushughulika na mambo ya michikichi. Sasa uko umuhimu tupige kampeni kubwa sana kuimarisha zao la alizeti kwenye mikoa hasa ya kati ambapo zao hili linastawi.

Mheshimiwa Spika, pia tuangalie namna ya kuwasaidia hawa wakulima na wafanyabiashara wadogo wadogo wanaokaa na mafuta barabarani. Waziri wa Viwanda aangalie namna anavyoweza kuwasaidia mafuta hayo yakakusanywa lakini yakawekwa kwenye mzunguko yakiwa na viwango. Jambo hili tumekuwa tukilizungumza sana kwenye Wizara ya Viwanda tunasema kwamba mafuta ya kula yanatumia fedha nyingi za kigeni, jambo hili likifanywa vizuri tunaweza tukaokoa fedha za kigeni lakini pia tukainua uchumi wa Watanzania na Taifa letu likawa limekaa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukijikomboa katika sekta ya kilimo, tutakuwa tumepunguza pia umaskini. Kwa hiyo, dhana ya umaskini na yenyewe itakuwa imepewa suluhisho la kudumu. Tumeona juhudi mbalimbali zimefanyika, kuna mradi ule wa matrekta pale Kibaha, ingeangaliwa namna ya kuweza kusaidia wakulima wetu wa vijijini na pia tuweze kuwapanga vizuri ili waweze kulima maeneo makubwa kidogo na walime kilimo chenye tija.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni sekta ya elimu. Tunaipongeza Serikali kwa kazi kubwa ambayo imefanyika. Sisi tunaotoka majimbo ya vijijini hiyo kazi tunaiona. Kwa hiyo, mtu anayesimama hapa Bungeni akasema hajaona kazi hiyo wengine sisi tunamshangaa.

Mheshimiwa Spika, isipokuwa pamoja na kuendelea kutoa Elimu Bila Malipo yako mambo makubwa ambayo yamefanyika, kwa mfano, ujenzi wa maabara lakini baadhi yake bado hazina vifaa. Kwa hiyo, naomba vifaa vya maabara vipatikane, technicians na walimu kwa sababu tunasema elimu ndiyo ufunguo wa maisha. Kwa hiyo, sekta ya elimu tukiimarisha tutaweza kupiga hatua kubwa.

Mheshimiwa Spika, si hivyo tu bali iko mikoa na jamii ambazo ziko nyuma kielimu, kuna maeneo ambayo hata hayafikiki. Kwa hiyo, tunaomba Ofisi ya Waziri Mkuu ifanye tathmini na kuona maeneo hayo yanasaidiwaje na hizo jamii zinasaidiwa kwa kiwango kipi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitoe mfano rahisi tu, kuna pesa ambazo Serikali inatoa kusaidia kwenye shule kuboresha miundombinu lakini utakuta zile sehemu ambazo ziko nyumba hazipewi kipaumbele, unakuta mtu anacho halafu anaongezewa. Nashauri utengenezwe mkakati wa makusudi ili kuwe na uwiano wa elimu na jamii zingine zisije zikaachwa nyuma.

Mheshimiwa Spika, katika eneo hilo hilo, niipongeze Serikali kwa sababu Mkoa wa Singida tumepata kama shilingi
1.3 ambazo ziligawanywa katika kila Jimbo ili kufunika maboma. Hata hivyo, bado tunasisitiza kwamba Serikali iangalie namna ya kutenga pesa zaidi ili zile nguvu za wananchi zisiweze kupotea. Tumeona miradi kama hiyo ni mizuri sana, Mwenge umepata fursa ya kufungua miradi hiyo, viongozi wanakuja, Mawaziri, Waziri Mkuu, Rais, Makamu wa Rais wanapata nafasi ya kufungua miradi hiyo ambayo inasaidia kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu.

Mheshimiwa Spika, kwenye sekta ya nishati, kazi kubwa imefanyika, tunapongeza upatikanaji wa vyanzo vya umeme, ujenzi wa Stigler’s Gorge, Kinyerezi, Rusumo na maeneo mengine, kazi kubwa sana imefanyika na umeme huu ndiyo pia utasaidia viwanda. Kuna huu utekelezaji wa Mpango wa REA III wa usambazaji wa umeme vijijini na yenyewe imekuwa ni changamoto kubwa, yako maeneo ikiwepo Mkoa wa Singida ambao utekelezaji wake unasuasua sana. Kwa hiyo, tunaomba Serikali kwa ujumla wake iweze kuangalia jambo hili, Waziri mhusika ameahidi kwamba atafika na tunaamini kwamba atafika ili umeme huo uweze kupatikana.

Mheshimiwa Spika, kutokana na hilo napenda niseme tu comment moja kwamba mimi kwa mtizamo wangu wako watu ambao wamepewa madaraka hawaisaidii sana Serikali kwa maana ya kwamba Mawaziri wanapokuwa wanafanya ziara, Mawaziri wa sekta zote, yanafanyika maandalizi mazuri na wanapofika pale wanapata taarifa nzuri lakini sasa wakiondoka utekelezaji wake unakuwa ni changamoto. Kwa tunaomba jambo hilo liweze...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Kiula.

MHE. ALLAN J. KIULA: Naam!

WABUNGE FULANI: Muda umeisha.

MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)