Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujaalia afya njema tukaweza kuzungumza masuala mbalimbali ya nchi yetu. Pili, asubuhi wakati Mheshimiwa Baba Paroko Joseph Selasini akizungumza hapa kuna maneno aliyasema, niongezee kidogo katika yale aliyoyasema, nimuombe Rais wetu msikivu, kwa heshima na taadhima, haya yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza, kupitia kwa DPP wetu ambaye ana dhamana basi waweze kuwapatia dhamana Waheshimiwa Wabunge wenzetu ambao tumewakosa katika Bunge hili; Mheshimiwa Freeman Mbowe na Mheshimiwa Esther Matiko ili Bunge lijalo tuweze kujumuika nao. Pili, kupitia nafasi hiyohiyo, nimwombe tena Mheshimiwa Rais wale Mashekhe wetu ambao hawajapata dhamana mpaka leo nao wapatiwe dhamana ili waweze kuhudumia jamii yetu katika huduma za kiroho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine niipongeze TAMISEMI kwa kumaliza mgogoro wetu wa Hospitali ya Wilaya kule Tanga ambapo sasa ujenzi unaendelea. Vilevile pia nishukuru kwa Vituo vyetu vya Afya vya Makorora, Mikanjuni na Ngamiani navyo kwa kupatiwa fedha takribani shilingi bilioni 1.4 na hali inaendelea vizuri.

Mheshimiwa Spika, kwenye mchango wangu nizungumzie Serikali za Mitaa. Najua tunazo Serikali za namna mbili, tuna Central Government (Serikali Kuu) na tuna Local Government ambazo ni Serikali zetu za Kienyeji au Serikali za Mitaa. Mimi nilikuwa najua kazi ya Serikali za Mitaa kwanza ni kukusanya kodi, kutoa huduma bila ya kusahau kutengeneza ajira kwa wananchi wa eneo husika. Hata hivyo, sasa hivi Serikali zetu za Mitaa zimepokonywa vyanzo vya mapato kama property tax hata mabango ya biashara, imekwenda sasa wananyang’anywa mpaka uwakala wa barabara za vumbi, ukarabati na ujenzi wa mifereji lakini hata huduma za taa za barabarani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu shughuli hizi sasa zinapelekwa TARURA (Wakala wa Barabara) basi TAMISEMI ingefanya utaratibu ufuatao; hizo gharama za usafi wa mifereji na taa za barabarani nazo zingepelekwa TARURA ili kuzipunguzia Halmashauri zetu mzigo. Kwa sababu Halmashauri zinafanya shughuli kubwa sana, zinashughulika na masuala ya afya, elimu na masuala mengine ya huduma za kijamii. Kwa hiyo, naishauri Serikali kwamba TARURA ibebe mzigo wa huduma za usafi wa mifereji na taa za barabani lakini enough is enough hivi vyanzo vya mapato vya Halmashauri visichukuliwe vingine.

Mheshimiwa Spika, hata hili suala la uvuvi, Halmashauri zinapokea mapato katika uvuvi kutokana na ushuru wa samaki. Kwa bahati mbaya sasa katika hiyo operesheni, kumekuwa na tatizo kwamba wavuvi wanapokamatwa na nyavu ambazo haziruhusiwi wanatozwa faini mpaka shilingi milioni 2 kwa nyavu moja lakini cha kushangaza, nina mfano wa risiti hapa ambazo wametozwa wavuvi, navyojua mapato ya Serikali sasa hivi yanakusanywa kwa EFD machine, hizi risiti ukizitazama zimeandikwa kwa mkono. Nina mashaka inawezekana mapato haya yakavuja na ikawa ni mianya hii ya kutengeneza masuala ya rushwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine nalotaka kulizungumza ni kwenye uteuzi wa Wakurugenzi. Baadhi ya Wakurugenzi siyo wote wamekuwa wababe na wakati mwingine wanakuwa na kiburi. Nitoe mfano wa Mkurugenzi wa Jiji langu la Tanga, mimi upande mwingine ni Diwani wa kuchaguliwa katika Kata yangu lakini ameniandikia barua kwamba eti nimepoteza sifa ya kuwa Diwani kwa kukosa Ward Council sita. Naamini Mkurugenzi anajua Kanuni za Halmashauri, moja ya sifa za Diwani kupoteza sifa ni kutohudhuria vikao vitatu vya Mabaraza ya Madiwani (Full Council) bila taarifa siyo Ward Council sita. Nimeiandikia barua Wizara ya TAMISEMI lakini mpaka leo sijapata majibu. Vilevile Mkurugenzi hata kuniita labda akaniambia Bwana hili jambo ulilifanya kimakosa kwa sababu Kanuni hazisemi hivyo imeshindikana. Mimi niitake TAMISEMI kwanza inipe majibu ya barua yangu lakini Wakurugenzi nao tuwasimamie waweze kutoa ushirikiano mzuri kwa Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)