Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Eng. James Fransis Mbatia

Sex

Male

Party

NCCR-Mageuzi

Constituent

Vunjo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi ya kuwa mchangiaji wa kwanza siku ya leo.

Mheshimiwa Spika, nitajikita zaidi kwenye Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na mapendekezo yao na ushauri wao ni mzuri sana, nawapongeza Kamati. (Makofi) Mheshimiwa Spika, kwa kiasi kikubwa wamefafanua baadhi ya malengo na mwelekeo wa elimu yetu Tanzania. Lengo la Nne la Maendeleo Endelevu Duniani ni elimu bora, sawa, shirikishi kwa wote. Tunajiuliza leo hii, je, Sera yetu ya Elimu Tanzania na mitaala, muhtasari na vitabu vinaakisi mahitaji ya kusudio hili au lengo hili la dunia? Je, mahitaji ya msingi ya wanafunzi wetu, marupurupu ya walimu wetu, mazingira rafiki katika shule zetu, yanaweza yakaakisi lengo
hili la dunia?

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa sababu ukiangalia Sera yetu ya Elimu ya sasa hapa Tanzania na Mheshimiwa Waziri aliwahi kusema hapa Bungeni kwamba ina matatizo, tunajiuliza leo hii Tanzania tunafuata sera ipi ya elimu? Ni Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 au ni Sera ya Eimu ya mwaka 1995? Hii ni kwa sababu Sera ya Elimu ya sasa inasema elimu msingi ni miaka sita baadaye miaka minne lakini kuna pre-primary ambayo inakuwa ni miaka 11. Leo tunafata Sheria ya Elimu ya mwaka 1978, kwa hivyo elimu yetu inakuwa haina mfumo ambao ni shirikishi, bora na unaelekeza usawa kwa wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa sababu tumekuwa tunafanyia elimu yetu sample na majaribio ya mara kwa mara, kwa mfano, suala la Big Results Now, ninayo nakala yake hapa, ukiangalia yaliyokuwa yameainishwa humu ndani yalikuwa ni mazuri sana. Hata hivyo, kisoma taarifa hii ya Katibu Mkuu ya utafiti ya Wizara ya Elimu, ambayo ilikuwa inaeleza elimu yetu kwa miaka mpaka 2024, ukurasa ule wa pili inasema, tatizo kubwa tulilonalo katika elimu yetu ni masuala ya kimfumo, kuna upungufu mkubwa wa kimfumo. Ni Wizara inasema yenyewe. Ukienda mbele zaidi ukurasa wa 62 inasema: “Usimamizi na uendeshaji wa elimu, uliotajwa kwa kiwango kikubwa, ni chanzo cha matatizo ya elimu Tanzania.”

Mheshimiwa Spika, sasa hii ni Serikali yenyewe inasema hivyo, leo hii tunajiuliza, hivi kweli mfumo wetu wa elimu, taarifa ya Serikali za Mitaa hapa, ya Mheshimiwa Rweikiza ameiwasilisha vizuri; hivi masuala ya kisera, kimuundo, kiuendeshaji yako TAMISEMI au yako kwenye Wizara yenyewe ya Elimu? Je, Waziri wa Elimu au Katibu Mkuu wa Elimu na Katibu Mkuu wa TAMISEMI wanaingilia vipi katika usimamiza wa Maafisa Elimu katika ngazi za Mikoa, ngazi za Halmashauri na Wilayani na kwingineko?

Mheshimiwa Spika, tatizo hili kwa kiasi kikubwa, ndiyo maana maandiko matakatifu yanasema, watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa. Ninasema hivyo kwa sababu, ukiangalia Tanzania ya leo, product ambayo tunazalisha sasa hivi; ukichukua Elimu ya Msingi, Sekondari, mpaka Vyuo Vikuu, kwa mwaka tunazalisha watu zaidi ya 1,200,000. Ifikapo miaka kumi ijayo, tutakuwa na vijana zaidi ya milioni 12, hawajui waende wapi, kwa sababu elimu yetu haimfanyi huyu kijana akawa mbunifu, awe skilled akajua kabisa ninamaliza elimu kwa kiwango hiki, naenda wapi.

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa sababu ni mara nyingi na nime-check kwenye Hansard ya Bunge ya mwaka 2013, niliwahi kusema kwamba udhaifu ulioko katika Sekta ya Elimu hapa Tanzania ndiyo unaosababisha tabia ya Watanzania walio wengi wa kutokujiamini katika kufanya majukumu yao, kupotea kwa mila na desturi za Kitanzania, kumomonyoka kwa uadilifu miongoni mwa wafanyakazi wetu, kuporomoka kwa uwajibikaji, yako mengi ambayo yaliainishwa.

Mheshimiwa Spika, athari zake sasa nini? Zinasababisha nini katika elimu yetu? Athari zake ni pamoja na ugumu wa elimu yenyewe, huduma mbovu zinazotokea katika sekta mbalimbali, viwango duni vya ubora wa bidhaa hii inayozalishwa hapa Tanzania, uharibifu wa mazingira yetu, udhaifu katika kukabiliana na majanga ya aina mbalimbali hata namna gani tunasimamia TEHAMA yetu.

Mheshimiwa Spika, hii ripoti ukiisoma tufanye nini kwenye utafiti ili tujue tunaenda wapi, ukurasa wa 55 unasema, nchi za Afrika zimekubaliana kwamba 1% ya GDP yake iwekezwe kwenye utafiti, lakini taarifa ya Kamati inaonyesha hapa inasema ni asilimia 0.034 ndiyo inayotolewa kwenye utafiti, ambapo kutokana na GDP yetu utafiti peke yake, COSTECH wangetakiwa wapate one point two trillion kwa sababu ndio tunajijua tunataka twende wapi; lakini leo hii, wanapata shilingi bilioni 40 tu. Kwa hiyo, hapa kitakwimu ni kwamba tunaiua elimu yetu sisi wenyewe.

Mheshimiwa Spika, sasa ukiangalia Vyuo Vikuu, mathalan, nilikuwa naangalia kwenye utafiti, ukiangalia Vyuo Vikuu 28,000 duniani, kwenye Ranking Web of Universities; 28,077. Tanzania tuko wapi? Tanzania kitakwimu kati ya Vyuo Vikuu 28,000 mpaka 10,000 hapo katikati, Tanzania ndiyo tunaingia hapo kwenye University zetu tano tu. Tuko kati ya 5,000 mpaka 10,000. Ni kwamba sasa tuko kwenye dunia gani Tanzania? Yaani katika 5,000 bora hatumo duniani.

Mheshimiwa Spika, naomba tu kwa unyenyekevu mkubwa, Vyuo vyetu Vikuu ukiangalia mfumo wenyewe wa utoaji mikopo, hauoani na mikopo inarudishwa. Je, ule utaratibu ambao tulishawahi kuusema Benki, tukawa hata na Benki ya mikopo, watu wanaenda kukopa kule kwenye Benki moja kwa moja na mkaweka mfumo wa namna gani wa kurudisha hizo fedha ili mikopo yetu iweze ikawa ni endelevu umefikia wapi?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ubunifu uko wapi? Vyuo Vikuu vya Umma viko hoi bin taaban. Kwa mfano, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, tangu mwaka 2014 wale wanataaluma; kinaidai Serikali zaidi bilioni 16.1 na Wahadhiri hao, Wanataaluma wako kwenye hali ambayo ni ngumu sana, ambayo inaleta matatizo.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa ajira, zimefanyika teuzi mbalimbali kutoka kwenye Vyuo Vikuu, replacement yake ikoje? Ndiyo maana unakuta Vyuo Vikuu vyetu leo hii zaidi ya watu wenye umri wa wanataaluma Wahadhiri wenye miaka 70 na kuendelea, bado wanapewa ajira za mikataba katika Vyuo Vikuu na efficiency inakuwa kwenye hali ya namna gani?

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mazingira, kuna mtaalam mmoja aliwahi kusema kwenye dunia ya leo “with technology things are changing faster than we can imagine, knowledge is for free for those who loves it, an educated person is the one who loves knowledge and seek it.”

Mheshimiwa Spika, nimelisema hilo kwa sababu kama hatutakubali, tukarudi miaka ya 1980 ambako kwenye Kamisheni ya Jackson Makwetta, ambayo alipendekeza tufanye nini Tanzania; na mpaka miaka 13 baadaye ndiyo ikatoka sera ya kwanza ya mwaka 1995.

Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa kabisa, niiombe Serikali ya Awamu ya Tano, Mheshimiwa Rais, Dkt. Magufuli, aunde Kamisheni ya Elimu Tanzania kabla ya Taifa letu la Tanzania halijaangamia. Kamisheni ya Elimu ambayo itatuambia sisi humu ndani tunataka nini, Kamisheni ya Elimu itakayojadiliana kama Watanzania tunataka mfumo wa namna gani vijana wetu wajiendeleze; Kamisheni ambayo tutajua duniani kuko namna gani; Kamisheni itakayotuonyesha mfumo wetu wa elimu uwe namna gani; Kamisheni ambayo itatuonyesha Tanzania ya leo tunataka iende upande gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kumalizia kwa maneno ya Yeremia 22:29 inasema, “Ee nchi, nchi, nchi lisikie neno la Bwana.”

Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunisikiliza.