Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Kwanza naomba nichukue nafasi hii kwa dhati kabisa kuzipongeza Kamati zote mbili kwa namna ambavyo wamechambua na kuleta ripoti zao ambazo ziko mbele ya Bunge lako Tukufu. Kipekee kabisa, nimesimama mbele ya Bunge lako Tukufu kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kupitia Waziri wa Ardhi, Mheshimiwa Lukuvi, pamoja Naibu Waziri Mheshimiwa Mabula na sisi kule Mlalo tulikuwa na shamba la Mnazi Sisal Estate ambalo lilikuwa linamilikiwa na Kampuni ya Lemashi Enterprises, wawekezaji hawa kutoka Kenya, shamba hili lilitelekezwa kwa muda mrefu sana takribani miaka 15.

Mheshimiwa Spika, wewe ni mkongwe humu kulikuwa na Mbunge wa Jimbo la Mlalo, Mheshimiwa Charles Kagonji ndiye mtu wa kwanza kupigania shamba hili kurudishwa kwa wananchi. Kwa kipindi chake chote cha Ubunge wa Jimbo la Mlalo alishindwa. Hali kadhalika akaingia Mheshimiwa Brig. Ngwilizi naye amepambana lakini Mkenya yule pamoja na mianya mbalimbali ambayo alikuwa anaitumia kupitia watumishi ambao siyo waaminifu katika Halmashauri, Mkoa na Wizara kwa wakati huo mambo hayakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kipekee natoa pongezi hizi kwa Mheshimiwa Lukuvi, Waziri wa Ardhi, kwa kazi kubwa sana ambayo amefanya ndani ya kipindi cha mwaka mmoja na nusu tulifanikiwa kurudisha shamba lile mikononi mwa Halmashauri ya Lushoto. Hivi navyozungumza tayari tumeweka mwekezaji mwingine, sisi kwa bahati nzuri tumechukua shamba kwa mwekezaji na tukatafuta mwekezaji mwingine na tumepata mwekezaji mpya amelipa kodi zote stahiki Serikali zaidi ya shilingi bilioni 2.8 na ameshaanza kuwekeza zaidi ya trekta tano mpya ziko ndani ya shamba, ameweka excavator na kila aina ya mashine. Mashine zote ambazo zilikuwa zina process na kuchakata mkonge kwa maana ya kuanzia kukata mpaka mwishoni kutengeneza mchakato wa brushing amefufua mashine zote zile za Kijerumani ambazo zilikuwepo tangu miaka ya 1936. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, natoa pongezi hizi kwa sababu sasa wananchi wote wanaozungukwa na shamba lile ambalo linazunguka takribani kata tatu wamepata ajira za kudumu zaidi ya wananchi 330 lakini ambao wapo wamepata ajira siyo za kudumu za kwenda kukata mkonge wengine kwenda kupalilia kulima na kadhalika. Kwa hiyo, unaweza ukaona kwamba ni kwa kiasi gani uchumi wa Halmashauri ya Lushoto ulikuwa umelala kwa kipindi kirefu kwa sababu tu ya kumpata mwekezaji ambaye hakuwa sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba hili nilizungumze kwa uwazi sana, mashamba ya mkonge tunapoyazungumza ni makubwa sana, kwa mfano hili Shamba la Mnazi ni takribani heka 4,100 lakini mwekezaji huyu alikuwa amewekeza katika heka 500 tu. Kwa hiyo, shamba lingine lote likageuka pori ambalo limekuwa makazi ya nyoka baadhi ya wafugaji kulitumia kwa ajili ya shughuli ya ufugaji. Hata haya mashamba tunayoyazungumza katika Mkoa wa Tanga kwa maana ya Wilaya ya Korongwe na Muheza ambapo bado kuna mashambapori mengi unakuta hawa wawekezaji wanalima katika upande wa barabara. Kwa hiyo, unapopita huku barabarani unaona kuna shughuli zinaendelea lakini kimsingi zile shughuli ni kiini macho wanaweka tu hekari za mwanzoni barabarani lakini huko pembezoni ni machaka makubwa sana ambayo yamegeuka kuwa msitu. Kwa hiyo, nitoe rai sana kwa Wizara kwamba iendelee bado tunayo mashamba zaidi ya 36 ambayo hayaendelezwi katika Mkoa wa Tanga.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)