Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Frank George Mwakajoka

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia. Napenda nizungumzie sana kuhusiana na suala la kilimo hasa kilimo cha mazao ya chakula. Najua kabisa kwamba Watanzania wote wanajua kwamba mchango wa kilimo kwenye pato la Taifa ni mkubwa na mazao haya yanategemewa sana na Watanzania wote na hata leo tuko humu ndani ya Bunge tunaonekana tuko vizuri na tunachangia ni kwa sababu tumepata chakula.

Mheshimiwa Spika, imeonekana kabisa kwamba Serikali haijatilia mkazo kabisa kuhakikisha kwamba inawasaidia wakulima hasa wakulima wa mazao ya chakula. Najua kabisa asilimia 65 ya Watanzania wanategemea kilimo, lakini huwezi kuamini pamoja na kilimo kuchangia asilimia 30 ya pato la Taifa, lakini uwekezaji kwenye kilimo umekuwa chini ya asilimia mbili. Kwa hiyo, ninachotaka kuzungumza ningeomba sana kwamba Serikali ijaribu kuangalia ni namna gani inaweza ikawekeza kwenye kilimo hasa kilimo cha nafaka.

Mheshimiwa Spika, imetokea sasa hivi kauli mbalimbali zimekuwa zikitolewa. Nakumbuka mwaka jana Mheshimiwa Rais amejaribu kuzungumzia akasema kwamba mazao ya chakula siyo biashara, lakini ukweli tu ni kwamba watu wamewekeza fedha nyingi sana, kuna watu wanavuna mpaka tani 80, wanavuna tani 200, wanavuna tani 300, kwa ajili ya mazao ya chakula lakini leo kuna kauli zinasema kwamba mazao ya chakula siyo biashara.

Mheshimiwa Spika, ukijaribu kuangalia kwenye upande wa pembejeo za kilimo mwaka jana wamesema kwamba wataagiza pembejeo kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wakulima waweze kupata pembejeo kwa bei ndogo, lakini ukweli tu ni kwamba katika mwaka ambao tumewahi kununua pembejeo kwa bei kubwa ni mwaka huu ambapo pembejeo zimepanda kwa asilimia zaidi ya 20 kwa kipindi hiki. Kwa kweli tunaomba Serikali ijaribu kuangalia ni namna gani inaweza ikaboresha pembejeo hizi ikaweka ruzuku kama zamani ilivyokuwa inafanya. Serikali ya Chama cha Mapinduzi katika miaka iliyokuwa imepita Mheshimiwa Kikwete na Mheshimiwa Mkapa walikuwa wameweka ruzuku kwenye pembejeo za kilimo, lakini sasa ruzuku imeondolewa na biashara inafanyika holela, Serikali inachokisema ni kwamba imeamua kusimamia pembejeo hizi kwa kuweka bei elekezi.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, bei elekezi imekuwa ni kiini macho, kwa sababu bei elekezi Serikali inasema lakini haijachukua tathmini ya kutosha kuangalia ni namna gani soko la pembejeo likipanda kwenye soko la dunia, haijaangalia mafuta yakipanda ni namna gani inaweza kuwasaidia wakulima hawa ili waweze kupata pembejeo kwa bei rahisi, kwa hiyo kumekuwa na tatizo kubwa sana. Kwa mfano mwaka jana walisema pembejeo za kilimo watu watanunua kwa mfano kama DAP walisema watanunua kwa Sh.58,000 lakini kutokana na bei za Soko la Dunia ilipanda mpaka kufika Sh.65,000 mpaka Sh.67,000, Urea pia ni hivyo hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunachoomba ni kwamba, Serikali iweze kurudisha mfumo wa ruzuku kwenye pembejeo za kilimo hasa kilimo cha nafaka ili kuhakikisha kwamba wananchi wote ambao wanalima mazao haya, waweze kupata ruzuku ili kuhakikisha kwamba mazao haya wanalima kwa urahisi lakini pia wanauza mazao yao kwa urahisi. Kama haitoshi imeonekana kwamba bei ya soko la mazao ya chakula sasa hivi imekuwa ni tatizo kubwa sana na hili tatizo siyo kwamba wakulima wamesababisha, Serikali ya Chama cha Mapinduzi ndiyo imesababisha tatizo hili la bei ya chakula kuwa chini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka 2017/2018, tulikuwa tumepata soko zuri kabisa Kenya, lakini Serikali ikazuia mipaka kwamba hakuna kuuza mazao nje na badala yake mazao hayakuuzwa nje, badala yake masoko haya yakahamia katika nchi zingine sasa hivi Wakenya wanakwenda kununua mahindi Zambia na Malawi, sisi tumekosa soko kwa sababu Serikali ilizuia mazao yasitoke. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini mwaka huu bado mwaka huu imetokea tatizo lingine...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

SPIKA: Muda hauko upande wako

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, dakika mbili na nusu hii.

SPIKA: Tayari dakika tano, muda unaenda haraka kweli, ahsante sana.