Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018

Hon. Suleiman Ahmed Saddiq

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mvomero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018

MHE. SULEIMAN A. SADDIQ – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA VIWANDA, BIASHARA NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba nikushukuru sana wewe kwa kunipa nafasi tena kuja kumalizia shughuli ambayo tumeianza asubuhi ya leo. Pia naomba nikushukuru kwa mara ya pili kwa jinsi ulivyoweka mstari katika suala lililozungumzwa na Waziri wa Fedha. Waziri wa Fedha ameleta habari njema, amezungumzia kwamba ile refund ya industrial sugar ya 15% Serikali imeanza kulipa na wameanza kulipa tokea Desemba na wewe ukaweka mkazo hivi hakuna watu wenu wakalieleza hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Kamati tulilizungumza hili muda mrefu, tulipata vilio vya wenye viwanda, wakasema mitaji yao imeganda, imekwama, wanashindwa kuendelea na uzalishaji na wengine wakatishia hata kufunga viwanda. Leo Serikali imefanya kazi kubwa, wameanza kulipa; Kamati ilikuwa ipaswe kuambiwa mapema. Mheshimiwa Dkt. Mpango tunakushuru sana kwa hili na niishukuru sana Wizara kwa kuanza kulipa na tuwaombe kama Kamati waendelee kulipa, bado kuna wengine wamebaki endeleeni kuyafanyia kazi. Hii ni Serikali sikivu na sasa ni kweli Tanzania ya viwanda imeanza kusikilizwa, hongera sana kwa Mheshimiwa Dkt. Mpango na hongereni sana Wizara zote zinazosimamia jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kuwashukuru wachangiaji wote waliochangia katika hotuba ya Kamati ya Viwanda na Biashara, niwashukuru Wabunge wote lakini naomba kwa sababu ni wachache mno niwatambue. Waliochangia kwa kuzungumza ni Waheshimiwa Wabunge 15; Mheshimiwa Mwambe, Mheshimiwa Kishimba, Mheshimiwa Kiteto, Mheshimiwa Musukuma, Mheshimiwa Mndolwa, Mheshimiwa Lema, Mheshimiwa Millya, Mheshimiwa Nsanzugwanko, Mheshimiwa Amon, Mheshimiwa Komu, Mheshimiwa Mbatia, Mheshimiwa Mwigulu, Mheshimiwa Genzabuke na Mheshimiwa Mollel pamoja na Makamu Mwenyekiti Kanali Masoud. Nawashukuru sana wote hao waliochangia kwa kuzungumza na kuna mmoja amechangia kwa maandishi Mheshimiwa Peter Lijualikali. Nawashukuruni sana wote ambao mmeunga mkono na kuchangia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ambao yamezungumzwa sana katika michango ya Wabunge ni maeneo ambayo tumeyasema sisi kama Kamati, maeneo ambayo Kamati imeiomba Serikali iyafanyie kazi haraka, maeneo ambayo Kamati ilishaomba Serikali au ilishawashauri Serikali kuyashughulikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza lilikuwa ni suala la VAT refund ya 15%; wapo Wabunge wamelizungumza sana hili na Serikali imeanza kulishughulikia. Naipongeza sana Serikali katika eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni viwanda vilivyobinafsishwa; hapa katika eneo la viwanda vilivyobinafsishwa kuna shida kidogo. Kuna shida kwa sababu zile data ambazo tumeletewa sisi kama Kamati na hizi data ambazo zinaendelea kutolewa haziendi sawa. Sisi Kamati na Wizara tunatakiwa wote tunyooshe mstari. Waziri anaposema viwanda vinavyofanya kazi vizuri sana 68 sisi tunasema sio 68, kwa hivyo hatuendi vizuri. Nitaomba Mheshimiwa Waziri tukae tuyaweke sawa haya mambo na Kamati ilikuwa inaomba sana tupate data za uhakika kwa sababu nia na madhumuni wote twende kwenye mstari ulionyooka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili la viwanda vilivyobinafsishwa limebeba eneo kubwa la uchumi wa nchi yetu. Viwanda hivi vingine vinakosesha ajira, Serikali inakosa mapato, lakini kubwa zaidi Watanzania wanakosa bidhaa. Viwanda hivi vingine vilikuwa vina mitaji, wengine walikuwa wana business plan nzuri, wengine wamekopa mabenki, leo viwanda vingine havipo na mashine hazipo. Kwa hiyo, tunaomba eneo hili Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia Serikali muwe sikivu sana katika eneo hili. Tunaomba maazimio yetu yafanyiwe kazi kwa ubora wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo limezungumzwa sana ni suala la Liganga na Mchuchuma. Kamati ilishauri kwamba suala hili linahitaji uwekezaji mkubwa na Kamati imeshauri kwamba kama inawezekana tungeanza kuuza raw material, ile raw material tukianza kuuza gharama zitakuwa ni ndogo lakini tukisema tujenge kiwanda gharama bado ni kubwa, kutahitajika gharama za kila aina. Kwa hiyo, ni matumaini yetu kwamba suala hili Serikali imeliona na nashukuru kwa majibu mazuri ambayo Mawaziri wameanza kuyatoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo Wabunge wamelizungumza zaidi ni mazingira ya kufanyia biashara. Ni kweli kulikuwa na tatizo ambalo ni kubwa, Serikali imekuwa sikivu, Mheshimiwa Rais ameshafanya vikao mbalimbali na private sector, Wizara wameshafanya mikutano mbalimbali na wadau na sisi kama Kamati tumeshashiriki kwenye baadhi ya mikutano yao. Ombi letu kama Kamati ile mikutano ya wadau iendelee, iwe ni mikutano ya mara kwa mara. Tutakuwa tunapata changamoto na kuzitatua haraka iwezekanavyo. Vikao kama vile inaonekana vimesitishwa, tunaiomba sasa Serikali ianze kuvifufua vikao vile na mazungumzo ya mara kwa mara yaendelee kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kuipongeza Serikali, zipo tozo ambazo zimeanza kuondolewa. Zipo tozo ambazo zilikuwepo kwenye blue print wameanza kuzianyia kazi kwa upande wa OSHA zipo tozo tano zimeondolewa. Kwa hiyo, Kamati yale ambayo imependekeza yameanza kushughulikiwa lakini bado tunahitaji iende kwa kasi zaidi kwa sababu malalamiko ni mengi kuliko vile yanavyoshughulikiwa. Inaonekana kuna mwanga kwamba kazi imeanza kufanyika na naipongeza sana Serikali. Naipongeza sana Serikali kwa sababu sasa hivi Mheshimiwa Rais ametuwekea Wizara ya Uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hii Wizara ya Uwekezaji tuna matumaini makubwa kama Kamati kwamba, tutafanya kazi kubwa, tutapata wawekezaji wengi na wawekezaji wengi watakuja kwa sababu Serikali ni sikivu. Katika hili nimpongeze Mheshimiwa Waziri Angella leo amezungumza maneno ya maana sana na ameunga mkono juhudi zote za Kamati, kwa pamoja tutafika Mheshimiwa Waziri karibu sana kwenye Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mengine limezungumzwa suala la wafanyabiashara kukaa pamoja, hili lilianza kufanyika; Serikali ilianza kukaa pamoja na wafanyabiashara. Tunaomba utaratibu ule uendelee na Mheshimiwa Rais tunampongeza na yeye mwenyewe kwa juhudi zake, alishakaa na taasisi mbalimbali, alishazungumza suala la kodi na tozo na matumaini yangu kwamba mambo haya sasa yanaanza kushughulikiwa hatua kwa hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la Kiwanda cha Urafiki, kiwanda hiki kinasuasua muda mrefu na kiwanda hiki kimepata mwekezaji ambaye toka ameingia ni hasara, hakuna faida yoyote kwenye Kiwanda cha Urafiki. Ajira zilikuwa 2,000, sasa hivi kuna ajira chini ya 400; kiwanda kilikuwa kinapata faida, sasa hivi ni hasara kwa miaka na miaka. Kamati inaomba juhudi za haraka zichukuliwe, Urafiki ilikuwa inazalisha mazao mazuri, vitenge vizuri, Watanzania wengi walikuwa wanakimbilia pale. Tunaomba juhudi za haraka zichukuliwe ili Kiwanda cha Urafiki kirudi kwenye enzi za Mwalimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la bajeti ya usimamizi wa mazingira kwa kweli haiendani na kasi ya uharibifu wa mazingira. Katika hili naomba nimuunge mkono Mheshimiwa Waziri January, amezungumzia hapa kwamba Wabunge waliochangia ni watatu; jamani mazingira ndio uhai wa viwanda Tanzania, mazingira ndio kila kitu katika nchi yetu. Leo tunapoonyesha kwamba hatutambui mazingira tunawakatisha tamaa wataalam na tunaikatisha tamaa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba sasa Wabunge wajue kwamba bila ya mazingira hakuna viwanda, bila ya mazingira tunaharibu nchi yetu, mazingira tukiyahifadhi vibaya hata kilimo kitaharibika. Wabunge wapewe elimu zaidi Mheshimiwa Makamba waweze kutambua nini maana ya uhifadhi wa mazingira. Mheshimiwa January nakuunga mkono sana katika hili, sisi kama Kamati tumeridhika na kauli yako elimu bado ni ndogo hasa kwa Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba bajeti itengwe ya kutosha katika eneo la uhifadhi wa mazingira ili tuweze kudhibiti uharibifu unaoendelea. Uharibifu ni mkubwa sana kwenye migodi, viwanda, mito na vyanzo vya maji. Suala la tabianchi linatumaliza kwelikweli, kwa hiyo tunaomba sana haya mambo yote yaende pamoja lakini bajeti ni ndogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge ambao wamezungumzia haya, lakini Mheshimiwa Lema amezungumzia sana suala la Kiwanda cha General Tyre, General Tyre sisi kama Kamati tumelizungumza sana na zipo ahadi mbalimbali za Serikali. Sisi kama Kamati tunatilia mkazo zile ahadi za Serikali zifanyiwe kazi haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanda cha General Tyre kinapoteza mapato, Watanzania wanakosa matairi bora, ajali barabarani ni nyingi na mara nyingi sana Kamati imejifunza mali zinazozalishwa Tanzania zina ubora wa hali ya juu. Bidhaa za ndani ya nchi yetu zina ubora wa hali ya juu ukilinganisha na bidhaa kutoka China, India na mataifa mengine. Kwa hiyo, Watanzania wanapenda sana bidhaa za ndani na tuendelee kuzisimamia ili Watanzania wapate kilicho bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mengine yamezungumzwa katika eneo hili, sisi tunaomba tuyatilie mkazo kwa maana ya haya yote sasa yafanyiwe kazi kwa hatua zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo pia tunaomba lifanyiwe kazi ni suala la gharama za uzalishaji. Suala la gharama za uzalishaji wataalam watusaidie, viwanda vya Tanzania vinaonekana gharama za uzalishaji zipo juu na kuna mifano hai kuanzia kwenye sukari, chuma, mabati na ndio maana leo mabati kutoka China yamezagaa Tanzania, wanasema ni mabati feki kwa sababu ni mabati ya bei nafuu. Gharama za uzalishaji ndani ya nchi yetu zimekuwa juu, tunaomba kikosi kazi cha wataalam wakishirikiana na Wizara ya Fedha walifanyie kazi hili ili tujue kuna tatizo gani, kuna shida gani katika eneo hili ili wale ambao wana viwanda waweze kusaidiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo jambo ambalo tunatakiwa sote kwa pamoja tulione na tulifanyie kazi. Vipo viwanda vilivyobinafsishwa leo vimekuwa ni viwanda vya mfano vinatoa gawio kubwa kwa Serikali. Kamati inashauri viwanda hivi vilindwe, mfano, viwanda vya sementi, viwanda vya sigara, viwanda vya mabati kama ALAF na viwanda hivi vyote vya bia kama Serengeti, TBL na hawa ambao wanatoa gawio ni viwanda ambavyo vimebinafsishwa pamoja na viwanda vya sukari vinavyofanya vizuri Serikali ikae na wadau.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ilipotembelea wadau wana dukuduku, wadau wale wana mambo yao, tusipokaa nao tutawakatisha tamaa na gawio litashuka, uzalishaji utashuka na mapato ya nchi yatapungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali yule ng’ombe anayetoa maziwa mengi tuendelee kumlea, tumpe majani mengi ili aendelee kutoa maziwa mengi, huo ndio wito wa Kamati. Pia wale ng’ombe ambao hawatoi maziwa, tuendelee kutafuta namna yoyote ya kuhakikisha na wale ng’ombe wanaendelea kutoa maziwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa sababu viwanda vilivyobinafsishwa 156 asilimia 70 ya viwanda hivi vikifanya kazi, Taifa litapata ajira mapato ya nchi yataongezeka. Hapa Wabunge wengi wameshauri Mheshimiwa Spika aunde Kamati maalum ya kwenda kulisimamia hili na sisi kama Kamati tulisema hatuna tatizo na hilo, uamuzi ni uamuzi wa Spika. Kama inaundwa iundwe, tujue ukweli kwamba kuna nini katika jambo eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nimalizie kwa kusema kwamba zipo juhudi zinaendelea kufanyika na Kamati inaipongeza Serikali, zipo juhudi mbalimbali ambazo tayari tumeziona, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais anatekeleza kwa vitendo suala la Tanzania ya Viwanda. Kamati iko bega kwa bega na yeye na Kamati tutashirikiana na Serikali kuhakikisha kwamba tunasonga mbele kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba sasa Bunge lako Tukufu lipitishe mapendekezo yetu ya Kamati kuwa azimio la Bunge kama yalivyoletwa na Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.