Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika makuzi yangu nimefundishwa lugha ya staha, uvumilivu na heshima kwa wakubwa na wadogo. Namwomba Mungu azidi kunidumisha katika hulka njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hatua hii nazipongeza sana Kamati zote, ikiwemo Kamati yetu ya Biashara na Mazingira, kwa kazi kubwa ambayo wameifanya. Wametoa maoni na ushauri mzuri na sasa sisi Serikali kazi yetu kubwa ni kuyachukua maoni na ushauri na kuufanyia kazi kwa manufaa ya Watanzania ambao wametutuma wote tuje kwenye Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapojadili hoja humu Bungeni ni muhimu sana tukazingatia mambo muhimu ya msingi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi Julai, 2017 Bunge hili lilipitisha sheria mbili kubwa, Sheria ya Mamlaka ya Nchi Kuhusu Umilikiwa Maliasili ya Mwaka 2017 na Sheria ya Mapitio ya Majadiliano Kuhusu Masharti Hasi Kwenye Mikataba Inayohusu Maliasili za Nchi ya Mwaka 2017.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kipindi hicho hicho Bunge liliifanyia marekebisho makubwa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010. Lengo la hatua hizo lilikuwa ni kurejesha umiliki na udhibiti wa rasilimali zetu za Taifa kwa faida ya Watanzania walio wengi. Huo ndio msingi tulioutumia kufanya maamuzi ya kuifanyia mapitio ya kina baadhi ya mikataba, ikiwemo Mkataba wa Mradi wa Makaa ya Mawe wa Ngaka na Mkataba wa Mradi wa Mchuchuma na Liganga na miradi mingine ya aina hiyo. Tutakapokamilisha mapitio hayo tutatoa taarifa kwa Watanzania kupitia Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe ufafanuzi kuhusu eneo la biashara. Tunao mfumo uliopitishwa na Serikali wa kujenga mazingira rafiki ya kufanya biashara na katika maeneo kadhaa tumeanza kufanya utekelezaji hususani kwa mfano kwenye eneo la ushirikiano kati TFDA na TBS, hii ni mifano michache. Tunakamilisha mpango kazi utakaoanza rasmi utekelezaji wake 2019/2020 na kwa kufanya hivyo, tutapunguza sana gharama za ufanyaji wa biashara katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wa Mheshimiwa S. H. Amon wa kukutana na wafanyabiashara au waagizaji wa bidhaa kutoka nje, tumeuchukua na tutaufanyia kazi mimi na Mheshimiwa Mpango, Waziri wa Fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilipozungumzwa kuhusu uhasi wa balance of payments, nilisikitika kwa sababu ilihitajika sana uchambuzi wa kina. Taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwezi Julai, 2018 imeonesha Tanzania imeuza zaidi katika soko la SADC na mauzo yameongezeka kutoka dollar milioni 397 mwaka 2017 hadi dollar 413 milioni ambayo ni ongezeko la asilimia 12; na wakati huohuo tumepunguza uagizaji kutoka SADC kwa asilimia 12. Maana yake ni kwamba tumepata mafanikio chanya kwenye soko la SADC. Sasa hizi hatua bado tunaziongeza kwenye masoko mengine. Dalili hiyo inaonesha kwamba Viwanda vya Tanzania vimeanza kufanya vizuri zaidi ukilinganisha na viwanda vya nchi nyingine hasa katika bidhaa kama unga wa ngano, sabuni, saruji, mabati na bidhaa nyingine.

Mheshimiwa Menyekiti, aidha, hatua ambazo Serikali inaendelea kuzichukua hususani katika ujenzi wa reli, barabara za lami za kitaifa na mikoa, viwanja vya ndege, bandari, umeme, mawasiliano ya simu, maji, huduma za afya, elimu hususani wahitimu wenye ujuzi mbalimbali (skills) ambao watakuwa na michango mikubwa kwenye viwanda, ni hatua ambazo zitaboresha sana mwelekeo wetu kuelekea kwenye uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea ushauri wa Waheshimiwa Wabunge, kuhusu kuimarisha utendaji wa mashirika yetu kama SIDO, NDC, TEMDO, CAMARTEC, TIRDO, EPZA, TAN-TRADE, TBS na hata Wizara yetu ya Viwanda na Biashara, tutaufanyia kazi ushauri mzuri ambao Bunge limeutoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu viwanda, tunahamasisha viwanda na hata Waheshimiwa Wabunge tunawahamasisha wamiliki viwanda. Tumeweke vipaumbele vitatu muhimu; kipaumbele cha kwanza, ni viwanda vya kusindika au kuchakata mazao ya kilimo na mifugo; sekta ambazo zinategemewa na asilimia zaidi ya 75 ya Watanzania. Kipaumbele cha pili, ni viwanda vinavyozalisha bidhaa zinazotumika zaidi majumbani na kwenye sekta ya ujenzi ili kulihudumia vizuri zaidi soko la ndani; na kipaumbele cha tatu, ni viwanda vinavyoajiri watu wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana tushirikiane kwa pamoja, sisi wote ni Watanzania, tukianza kutoleana maneno machafu hatutasonga mbele. Tushirikiane kama Watanzania kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania ili Taifa letu liweze kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kidogo kuhusu viwanda vilivyobinafsishwa. Kati ya viwanda 156 vilivyobinafsishwa, viwanda 88 vinafanya kazi, sawa na asilimia 56, viwanda 68 havifanyi kazi. Kati ya viwanda 88 vinavyofanya kazi viwanda 64 vinafanya kazi vizuri, tena kwa faida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuonesha kwamba vinafanya kazi kwa faida kuanzia mwaka 2013 mpaka 2018 viwanda hivi hadi Oktoba, 2018 vimelipa kodi zaidi ya shilingi trilioni 4.6 TRA wanayo takwimu. Kati ya viwanda 64 visivyofanya kazi viwanda 20 vimefutwa kwenye orodha baada ya kubainika kwamba viliuzwa kwa rejareja; yaani viliuzwa mali mojamoja na vingine vimekosa sifa ya kuendelea kuitwa viwanda. Viwanda 14 tumeshavirejesha Serikalini baada ya wenye viwanda kutoonesha business plan ya kuvifufua na kuviendeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tumevichukua Serikalini ili tuvitafutie wawekezaji wengine ambao watakuwa na nia ya kuwekeza mtaji ambao utavifufua viwanda hivyo na kuendelea na uzalishaji. Viwanda 34 vinafuatiliwa kwa karibu utendaji wake kwa mujibu wa ahadi zao za kufufua uzalishaji ambazo wametuahidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu General Tyre; Serikali ilikamilisha tathmini ya kiwanda iliyoshauri kiwanda hicho cha General Tyre kifufuliwe kwa ubia na sekta binafsi kwa uwekezaji wa mitambo ya kisasa. Government Notice ya tarehe 11 Mei, 2018 ilikabidhiwa NDC na kiwanda rasmi kilikabidhiwa NDC tarehe 20 Disemba, 2018. Baada ya tathmini ya kina ya mali zote na madeni ambayo inaendelea NDC sasa itachukua hatua ya mwisho ambayo ni kualika makampuni yatakayokuwa tayari kwa ubia ili yalete maombi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Bunge lako Tukufu tuwe na subira wakati hatua muafaka hizi zinachukuliwa na hakuna haja ya kutoleana maneno ambayo yatafukuza hata wale ambao pengine wangeweza kuwa prospective kwenye uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mwelekeo mzuri kwa sekta zote. Sekta ya viwanda haiwezi kuendelea bila kuwa na uwekezaji kwenye sekta nyingine, huwezi kujenga viwanda bila kuwekeza kwenye sekta ya miundombinu. Hakuna eneo lolote la uwekezaji ambalo linaweza likavutia wawekezaji kama hakuna barabara inayofika kule, hakuna reli inayofika kule, hakuna umeme, hakuna maji, kwa hiyo hivi vitu vinategemeana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kuwa na viwanda vya Agro processing kama kilimo hakifanyi kazi vizuri; na ndiyo maana katika mkakati maalum wa maendeleo ya viwanda katika nchi hii tumesema lazima uwe na mkakati wa pamba hadi nguo; yaani C to C (Cotton to Cloth). Ili uweze kufikia malengo mahususi ya kutumia malighafi ya pamba vizuri zaidi ndani ya nchi lazima uwe na viwanda ambavyo vitatengeneza nguo kutokana na pamba inayozalishwa ndani ya nchi. Lazima kama unataka kuwa na viwanda vya mafuta;

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Namalizia Mheshimiwa Mwenyekiti…

MWENYEKITI: Malizia Mheshimiwa Waziri.

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima uwe na uzalishaji mzuri wa alizeti ili uweze kukamua mafuta ya alizeti vizuri. Kwa hayo ndiyo mambo ambayo tunayafanya na mwelekeo ni mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Kamati. Ahsante sana. (Makofi)