Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018

Hon. Agnes Mathew Marwa

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia. Kwanza namshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kunipa nafasi hii adhimu ya kuchagia siku ya leo ukizingatia na mimi ni mjumbe wa Kamati wa Miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa moyo wake wa dhati wa kujali Watanzania lakini pia wanyonge kwa kukubali kwa kutoa shilingi trilioni 15 kwa kipindi cha miaka mitatu kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania. Kipekee niishukuru sana Kamati yangu ya Miundombinu ikiongozwa na Mwenyekiti Mheshimiwa Kakoso na Naibu wake ambaye sasa hivi ni Meneja, kwa kufanya kazi nzuri sana ya kutuongoza na kutupitisha katika mambo mbalimbali kwa kushirikiana na Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli narudia tena kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Magufuli na kumpongeza sana sana. Kwa mtu kama mimi ambaye nimekuwa Mbunge kipindi cha kwanza kwa kutokea moja kwa moja kule Nyachalakenye tena nilikuwa muuza dagaa lakini sasa na mimi naweza kutunga sheria, kwa kweli ni jambo la kumshukuru Mungu na kumpongeza Rais wetu anaonyesha ni jinsi gani anavyofanya kazi na kuwakwamua Watanzania. Nami sasa ni msomi kati ya wasomi na nipo vizuri kwa sababu tulipoanza tu Kamati alitutumia wanasheria wakatufundisha, wakatupika tukaiva tukawa vizuri na sasa tunaweza kutunga sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kupitia Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa mafaniko makubwa, tukianza na mafanikio upande wa barabara na madaraja. Kwa upande wa barabara sasa Tanzania nzima barabara zinatengenezwa tena kwa kiwango cha lami; ni barabara ambazo zinapitika vizuri na zinasaidia kuunganisha sehemu moja na nyingine hata kufikia vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi cha nyuma kwetu kule Mara ilikuwa ukitoka Musoma kufika Dodoma ni lazima utumie zaidi ya siku tatu lakini ukifika pale Singida kulikuwa kuna watu wanawaimbisha watu mtaji wa maskini sasa hivi naamini kuna barabara ya lami na hawawezi tena kufanya matukio hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa madaraja kwa kweli Serikali imefanya kazi nzuri sana hata kama wale jirani zetu hawaoni wanasema mwenye macho haambiwi tazama basi Watanzania wapiga kura wanaona kwamba ni kazi kubwa sana imefanyika. Mfano ni kule kwetu Mkoa wa Mara kuna lile daraja na Mto Mara ambalo linaunganisha Tarime na Serengeti. Kwa kweli ilikuwa siyo sehemu nzuri na imeua sana watu lakini pia ilikuwa ni sehemu ambayo ulikuwa huwezi kupita mpaka uzunguke, hata uchumi ulikuwa huwezi kukua kutokana na kutumia muda mrefu barabarani kwa ajili ya kuzunguka kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Sasa hivi barabara ile imeunganishwa kutokana na lile daraja na limetengenezwa na wazawa tena wazawa wazalendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunawaomba sana ndugu zangu Watanzania na haswa wale mnaofanya shughuli kama hizo muwe wazalendo kama wale waliotengeneza Daraja na Mto Mara tutafika mbali sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee niishukuru sana na kuipongeza tena Kamati yangu ya Miundombinu kwa kazi nzuri tuliyoifanya. Tumeweza kuzunguka karibu mikoa yote ya Tanzania, tulizunguka mwezi mzima tukiwa tunafanya kazi za kuangalia minara simu, madaraja, barabara na ubora wake na viwanja vya ndege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tukiwa tunazunguka…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda umekwisha?

MWENYEKITI: Ndiyo maana yake, unga mkono hoja.

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)