Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018

Hon. Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii, I hope nina dakika 10?

MWENYEKITI: Wewe sema ukichoka utaniambia. (Kicheko)

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Sawa, nilitaka kuwa na uhakika nisikukwaze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwanza niwape hongera sana wenzetu wa Serikali hususani Wizara hii ya Miundombinu ambayo ni Wizara kubwa, niwape hongera Waziri, Naibu Mawaziri na watendaji wake wote kwenye Wizara hiyo. Kazi ni nzuri mnayoifanya lakini bado naamini wana nafasi ya kufanya vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitajikita kwenye mambo machache sana, la kwanza nianze na Wizara hii ya Miundombinu. Hii Wizara ni Wizara kubwa sana, hii ni Wizara ambayo ina taasisi zaidi ya 120, ni taasisi ambayo inasimamia mambo muhimu sana, na kusema kweli ni taasisi ambayo ndiyo kama mishipa ya damu kwenye uchumi wetu. Ukizungumza barabara ipo miundombinu, ukizungumza reli ipo miundombinu, bandari, mawasiliano, viwanja vya ndege, posta na simu, majengo, vivuko nchini, hali ya hewa na kadhalika bado yote haya yako chini ya Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niombe wenzetu wa Serikali mko hapa, hii Wizara ni kubwa sana. Pamoja na uwezo mkubwa walio nao Waheshimiwa Waziri na Naibu Mawaziri wa Wizara hii na Makatibu wao Wakuu bado ni jambo jema kama Mheshimiwa Rais ikimpendeza Mheshimiwa Rais Magufuli afanye kama tulivyoshauri kwenye Wizara ya Kilimo na Mifugo na kama alivyofanya kwenye Wizara ya Biashara na Viwanda. Aitenganishe Wizara hii ili kuwe na Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Uchukuzi na Mawasiliano kwa sababu Wizara hii ni kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa maoni yangu ni kwamba inafika mahali hata watendaji wanakuwa hawawezi kufuatilia mambo yote katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye jambo mahususi, hilo lilikuwa la jumla sana, nalo ni hili la ujenzi wa reli. Tunajenga reli ya Standard Gauge, jambo jema sana kwa uchumi wa nchi yetu; lakini niombe sana wenzetu na Mheshimiwa Waziri wa Fedha huko hapa, pendekezo lililopo ukurasa wa 31 ni pendekezo la msingi sana, kwamba ujenzi wa reli huu tunaouzungumza utakuwa na maana kiuchumi kama njia hii itajielekeza katika hiyo njia ya Tabora, Kigoma na Msongati na sababu zake wala huitaji kwenda shule kuzijua. Ni kwa sababu wenzetu wa DRC Mashariki yake na Kusini Mashariki yake wana mzigo mkubwa wana mzigo mzito ambao unahitaji kupita kwenye reli, ndizo economics zake tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na Waheshimiwa Wabunge reli msingi wake si kubeba bianadamu, reli msingi wake ni kubeba mizigo tena mizigo mizito. Hii dhana ya kwamba utatoka Dodoma utakwenda Dar es Salaam na mchicha wako na mayai yako ni mambo ya kizamani haya. Reli ni ya kiuchumi, tunaomba wenzetu wasimamizi Serikalini wakubaliane na agizo la ukurasa wa 31, tujikite eneo ambalo reli hii inakwenda kubeba mzigo mzito na huko si kwingine, ni Mashariki ya Demokrasia ya Congo na Kusini Mashariki ya Congo. Kwa maana ya kwamba reli hiyo ikitoka Tabora ikaenda Kigoma ikapata branch kwenda Msongati, kwa maana ya Uvinza kwenda Msongati - Burundi na nyingine ikaenda Kigoma - Lake Tanganyika mpaka Congo. Maana yake ni kwamba mzigo huo ambao una kisiwa kuwa zaidi ya tani milioni nne kwa mwaka utafanya reli hiyo iwe ni ya kiuchumi zaidi.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa niliseme ni reli ya TAZARA. Mimi ni mjumbe wa Kamati hii ya Miundombinu, hili jambo la reli tumelizungumza sana. Reli ya TAZARA au reli ya uhuru kuna mambo ambayo hayaeleweki vizuri, hii reli imefilisika. Ziko taarifa kwenye magazeti tumezisoma na nyingine zikimnukuu Mheshimiwa Waziri kuhusu namna wanavyoshughulikia jambo hili la TAZARA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali ni kwamba lazima mkataba huu wa TAZARA wautazame upya. Reli ya TAZARA inakufa na tunaambiwa sasa kuna wakodishaji eti wameanza kukodisha reli yetu ya TAZARA na ningependa pengine wakati wa kipindi cha bajeti kinachokuja Mheshimiwa Waziri wa Fedha mtueleze vizuri kwamba hii reli mnaikodisha kwa akina nani na kwa gharama gani, maana mahusiano yaliyokuwepo kati yetu na Zambia wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere na Mzee Kaunda yamebadilika sana. Kuna haja sasa kuanza kuitazama kiuchumi zaidi reli hii ya TAZARA na kuanza kuitazama kwa maslahi ya Tanzania zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa nilizungumzie ni viwanja vya ndege na ndege za ATCL. Hivi viwanja vya ndege ni vya kimkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na nilikuwa napenda niseme tu labda, kwamba nimekuwa Mkurugenzi kwenye Kampuni ya PUMA Energy kwa miaka saba. Ile Kampuni ya PUMA Energy ni Kampuni ya Serikali, kwa maana ya asilimia 50 za kampuni ile ni za Serikali. Kwenye viwanja vya ndege na mauzo ya mafuta ya ndege katika soko la SADC, PUMA Energy ina asilimia 86.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nazungumza na Mheshimiwa Waziri namwambia PUMA Energy ina asilimia 50 za Serikali tena za kihistoria Mheshimiwa Waziri akawa haelewi vizuri. Mheshimiwa Waziri wa Fedha hili liko kwako, huyu ni ng’ombe wa maziwa, kama alivyokuwa anaita Mheshimiwa Mwijage, huyu ni ng’ombe wa maziwa tumpe majani, tumtunze ili tuendelee kukamua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara ya ndege, si ndege zetu, hata ndege za majirani zetu na kampuni nyingine zinahitaji kuwa na uhakika wa mafuta yao na Kampuni ya PUMA Energy kwa miaka zaidi ya 13 sasa wameshikilia hilo soko vizuri na sisi kama Serikali tunapata asilimia 50 ya mauzo yao. Ni jambo jema na tunaomba sana wenzetu wa Serikali, Mheshimiwa Waziri wa Fedha hilo jaribio la kuwatishia kampuni yenu wenyewe asilimia 50 eti kulinyima leseni ni jambo ambalo naona kama ni aibu kidogo. Ni vyema mjiridhishe na ukweli wa mambo haya ili muweze kujua ni kitu gani mnachokizungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa nilizungumzie ni kuhusu kazi nzuri inayofanywa na Mamlaka ya Mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo la TEHAMA, jambo la mawasiliano ni jambo muhimu sana, ni jambo mtambuka. Ni maoni yangu kabisa kwamba kazi inayofanywa na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) hoja hii ya TEHAMA sasa ihame iende shuleni na kwenye vyuo; dunia imebadilika, dunia ni ya mawasiliano, dunia ni ya mitandao. Ushauri wangu kwa Serikali, ingekuwa ni jambo jema sana sasa Mamlaka hii ya Mawasiliano tuihuishe tui-link na vyuo vyetu na shule zetu ili sasa suala la kujifunza juu ya mitandao na TEHAMA katika shule zetu liwe jambo la msingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa nilizungumzie suala la barabara. Iko sera ya dhahiri ya barabara; kwamba sera yetu ya ujenzi wa barabara kama ilivyoainishwa kwenye ilani ya uchaguzi ya CCM ni kuunganisha mikoa na mikoa. Hata hivyo bado kuna mikoa michache katika nchi yetu haijaunganishwa kwa mujibu wa sera hiyo ya barabara. Mikoa hiyo ni pamoja na Mkoa wa Kigoma na Mkoa wa Katai. Tunawaomba wenzetu wa Wizara ya Ujenzi acheni kuanzisha miradi mipya, kamilisheni miradi ambayo mmeshaianza ili barabara hizi zikamilike. Haingiii akilini wanaanza miradi mipya wakati miradi ya zamani bado haijakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii barabara toka Nyakanazi mpaka Kabingo huko Kakonko ina mwaka wa kumi haijakamilika, leo hii barabara kutoka Kidahwe kuja Kasulu ina mwaka wa 11 haijakamilika, acheni kuanzisha miradi mipya tukamilishe miradi iliyopo. Tunaishukuru Serikali na wewe Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa jitihada mlizozifanya kupitia wenzetu wa African Development Bank kwa mradi mkubwa wa barabara kutoka Kabingo – Kibondo – Kasulu mpaka Maruku kwenda Burundi. Ni juhudi kubwa nzuri lakini tunaomba zisimamiwe ili kazi hiyo iishe. Ni kilometa 261 na kwa kawaida tunadhani ndani ya miaka mitatu/minne au mitano inaweza ikawa imekamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine katika ujenzi wa miundombinu ni suala la umeme. Ningependa kujua, maana umeme nao ni miundombinu vilevile, ningependa kujua ujenzi wa Hydro ya Malagarasi umefikia wapi ambao hatimaye umetuingiza kwenye mpango huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, najua muda wangu unakimbia, ni kuhusu jambo ambalo limezungumza na Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda na Biashara na kuna Mheshimiwa Mbunge mmoja amelizungumza na mimi pia napenda kuliunga mkono. Tumeambiwa, kwa mujibu wa report ya Kamati, kwamba kuna viwanda 156 vilibinafsishwa, viwanda kama 50/56 vinafanya kazi na viwanda vingine 100 havifanyi kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninashawishika kukubaliana kwamba kuna haja sasa Bunge hili liunde Kamati Maalum, si lazima iwe Kamati Teule, iundwe Kamati Maalum isaidiane na wenzetu wa Wizara ya Viwanda na Biashara ili tuweze kujua hivi viwanda 100 plus vilivyobinafsishwa hatima yake ni nini? Otherwise itabaki ni wimbo tu kila siku viwanda, viwanda ambavyo havifanyi kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo Tume ikiundwa inakuwa ya Kibunge tu wala si lazima iwe teule. Iwe Tume Maalum ambayo itakuwa na Waheshimiwa Wabunge wenzetu wachache pamoja na wenzetu wa Kamati ya Biashara na Viwanda, wapitie viwanda hivyo 100 plus ambavyo vimebinafsishwa lakini havifanyi kazi. Vinginevyo huu ni mwaka wa tatu, ni hadithi kila siku, kwamba viwanda, viwanda, lakini viwanda vyenyewe havifanyi kazi kama ambavyo tungetarajia vifanye kazi viweze kuingiza mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ningependa kuzungumzia huu mradi wa chuma wa Liganga na Mchuchuma. Sisi wachache ambao tumebahatika kufika pale, ukifika Liganga, Mchuchuma na pale Mbamba Bay utaona Mwenyezi alikuwa na makusudi yake. Liganga ni mlima, mlima wote wa Liganga umejaa chuma, chini ya mlima ule kuna mto mkubwa. Ukienda kilometa 32 ukitoka Ludewa unakutana na eneo linaitwa Mchuchuma. Mchuchuma ni mto mkubwa sana na eneo lote la Mto limejaa makaa ya mawe, ni kama Mwenyezi Mungu alisema ninawapa makaa ya mawe mpate moto wa kuyayeyusha na maji ya Mto Mchuchuma uweze kupoza chuma chenu hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa, ukienda Kusini Mashariki kuna Bandari ya Mbamba Bay, ni kama triangle una chuma, una makaa ya mawe na una bandari ya Mbamba Bay. Sasa kwa nini Serikali hamchukui hatua za makusudi …. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)