Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018

Hon. Zainab Mndolwa Amir

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018

MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia katika taarifa hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuipongeza Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira kwa taarifa yetu nzuri, pia naomba mapendekezo yaliyopo Serikali, iyafanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ubinafsishwaji uliofanywa wa viwanda zaidi ya 156, lakini ni vichache tu ambavyo vinafanya kazi. Ushauri wangu kwa Serikali ni kwamba, tunaomba vile viwanda ambavyo havifanyi kazi, kwa sababu wamiliki wake wamevigeuza matumizi na wengine wamekwenda kukopa fedha kwenye mabenki na kufanya biashara ambazo hazihusiani na mikataba walioingia, tunaomba Serikali iunde Kamati Maalum ya kuvichunguza viwanda vile na kuvirudisha Serikalini ili kuweza kupatiwa wawekezaji wengine kuweza kuviendeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna tatizo katika viwanda ambavyo vinazalisha vinywaji baridi, tumetembelea viwanda vingi lakini changamoto kubwa ni uingizwaji wa sukari ya viwandani, sukari ya viwandani haipatikani hapa nchini, huagizwa nchi za nje na Serikali ilipanga tozo kwa viwanda hivyo ambavyo vinatumia sukari ya viwandani asilimia 15. Wakati vinaingiza vinakatwa tozo ya asilimia 15 na Mamlaka ya Mapato (TRA), lakini sasa hivi ni takribani miaka mitatu Serikali hiyohiyo imechukua fedha za wenye viwanda haijarudisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mabilioni ya shilingi wenye viwanda wanadai, na tulikwenda katika viwanda hivyo wakatuonesha barua mbalimbali walizoziandika ambazo wameomba Serikali iwarudishie kwa sababu fedha hizo walizikopa katika taasisi mbalimbali hapa nchini na zinatozwa riba, kwa hiyo Serikali imeshikilia fedha yao takribani miaka mitatu sasa hivi. Kwa hiyo Serikali kama Serikali tunahamasisha, wanahamasisha uchumi wa viwanda hapa Tanzania lakini yenyewe pia inakwamisha kwa upande mwingine kwenye viwanda vyetu kuweza kuendeleza viwanda kwa kushikilia fedha ambazo zinatumika kwenye viwanda hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali tunaomba wale wenye viwanda ambao fedha zao walizoziingiza katika sukari ya viwandani zirejeshwe kwa wakati ili ziweze kutumika katika mitaji yao kwa sababu walilalamika sana wakasema na mitambo mingine imesitishwa kwa sababu hawana mtaji wa kutosha. Pia kama inawezekana, waweze kusitisha utozaji ule, Serikali ianzishe viwanda vya ndani ambavyo vitazalisha sukari ya viwandani kuliko kuagiza halafu wanatozwa tozo hawazirejeshi kwa wafanyabiashara hao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nazungumzia kuhusu utitiri wa kodi; utitiri wa kodi umesababisha baadhi ya wafanyabiashara kufunga biashara zao. Tunajua kabisa mtu akianza kufanya biashara anatakiwa alipe mapato kwa Serikali kwa kiasi anachopata, lakini sasa hivi Serikali inaanza kumtoza mtu mapato kabla hajaanza kufanya biashara. Naishauri Serikali iwapatie wafanyabiashara hao muda maalum (grace period) angalau ya miezi mitatu, wafanye biashara kisha ndiyo waweze kuwakadiria mapato yao, hiyo itasababisha watu kuweza kujua mapato wanayopata kwa wakati na kuwa na willingness ya kulipia mapato hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia pia katika Wizara ya Mazingira; tunaomba Wizara ya Mazingira kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kuwe na uvunaji endelelevu wa miti. Wizara iandae maeneo maalum ya kupanda miti ambayo itatumika katika viwanda ambavyo vinatumia malighafi ya miti kwa sababu kuna viwanda vingine vinatumia miti, lakini sasa unakuta ukataji wa miti unakuwa hovyo na kusababisha ukame katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Wizara itenge maeneo maalum ya kupanda miti ambayo itasaidia pia katika viwanda vyetu kama malighafi. Pia itasaidia katika matumizi ya nyumbani kama mkaa na kuni kwa sababu gesi tunaona ni ghali mno na watu hawawezi kutumia gesi ambayo ni ghali kwa sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kulikuwa na gesi asilia ambayo tunaomba Serikali iharakishe usindikaji wa gesi asilia ambayo itakuwa na unafuu zaidi kwa wananchi kuliko kuendelea kutumaini kwamba tutumie gesi tusitishe mikaa, mkaa kusitisha itakuwa ni ngumu, lakini Serikali ina mpango mkakati kupanga maeneo ambayo miti itapandwa, watu watakata miti na Serikali itapata mapato na watumiaji wa mkaa watatumia na pia mazingira yataboreshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kuzungumzia kuhusu matumizi ya mifuko ya plastiki; mifuko hii Serikali inataka isitishe kutokana na uchafuzi wa mazingira. Hata hivyo, tunaishauri Serikali kabla ya kusitisha itupe njia mbadala au mifuko mbadala ya kuweza kutumia, ambayo badala ya kutumia plastic sisi tutatumia mifuko ambayo inaendana na mazingira yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri pia Serikali katika ofisi ya mazingira wakati wa kampeni ya upandaji mti, naona sana miti inayopandwa ni ya vivuli, lakini naishauri Serikali tuwe na mkakati wa kupanda miti ambayo itakuwa ya matunda pia kwenye sehemu ambazo zina rutuba sio kupanda miti ya vivuli tu. Kwa hiyo, nashauri Serikali wakati wa zile kampeni za upandaji miti tuangalie sehemu zenye rutuba tuweze kupanda miti ambayo pia tunaweza kupata matunda, vivuli na kutunza mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri pia Serikali iweze kufuatilia haya yote katika Kamati yetu, kwa sababu mengi tulishayaeleza, ambayo tumependekeza Kamati yetu, tunaishauri Serikali iyatilie mkazo ili kuelekea Tanzania ya Viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)