Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018

Hon. Jumanne Kibera Kishimba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kahama Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwa kunipatia nafasi ya kuchangia kwenye Kamati hii ya Viwanda na Biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu na Wataalamu wote, pamoja na Wabunge wote wa Kamati hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisiwe mchoyo wa fadhila, nachukua nafasi hii ingawa si Wizara yake, kumshukuru Mheshimiwa Rais na kumpongeza kwa kuruhusu wachungaji na wafugaji pamoja na wakulima wanaokaa karibu na Hifadhi za Serikali kwa kuwaruhusu maeneo ambayo yana mapori ambayo hayana wanyama ili wananchi waweze kuyatumia wakati wa dharura, vilevile na vijiji 300 ambavyo vimeruhusiwa virasimishwe. Namshukuru sana kwa kupokea kilio cha wakulima na wafugaji cha muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naunga mkono mapendekezo ya Kamati, ila nina mawazo mawili/matatu ambayo yamo kwenye Kamati ningependa kuyafafanua na kuyaelezea vizuri, kama yataweza kuchukuliwa na kuwa msingi mzuri wa kuelekea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, ni suala hili la Liganga na Mchuchuma. Suala hili la Liganga na Mchuchuma lina takribani zaidi ya miaka 50 na kinachoonekana tunaweza tukaenda tena miaka mingine 50 kama hatukupata ufumbuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chuma ni bidhaa kama bidhaa zingine na ndani ya chuma cha Liganga kuna mchanganyiko wa madini mbalimbali. Kwenye mkutano wa madini Mheshimiwa Rais alieleza na analysis zilizomo kwenye mchanga ule. Pendekezo tulilonalo ni kwamba Serikali ichukue analysis za gharama za uzalishaji kama itajenga Kiwanda cha Chuma, ichukue analysis ya mali iliyomo mule ndani ya chuma ione kama inaweza kuu-peg ule mchanga kwa bei ili wanunuzi waweze kununua kwa kulipia Serikalini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana ya kuongea hili ni kwamba, wenzetu Waganda leo wanachimba crude oil kutoka Uganda wanapeleka Tanga kupitia hapa lakini wananunua petroli na dizeli kutoka nje kwenda Uganda. Ni kwamba ndani ya crude ile kuna vitu ambavyo kama watachenjua hiyo crude oil kule Uganda hawawezi kuisafirisha au hawawezi kutumia ile material nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na sisi kwa Liganga ni vizuri Serikali ikafikiria upya. Sababu nyingi za msingi ni kwamba chuma ni bidhaa kama bidhaa nyingine. Tunapoongea leo bei ya chuma duniani inaendelea kuanguka na hatujui ndani ya miaka kumi bei ya chuma itakuwaje maana chuma ni bidhaa ambayo inatumika na inakuwa recycle, sio kama chakula. Kwa hiyo hata kama tutang’ang’ania tunajua nini kitatokea baada ya miaka kumi. Ni vizuri Serikali ikafikiria kufanya analysis na kuanza kuruhusu chuma hicho Serikali iuze ili iweze kununua chuma kipya na kutumia au kupata pesa kwa ajili ya matumizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ni kwamba ndani ya chuma au ndani ya bidhaa zozote kama unataka kuzalisha hapa lazima uangalie matumizi ya yale makapi. Inawezekana sisi tunataka kutengeneza kweli hicho kiwanda, lakini kuna makapi na bidhaa nyingine ambazo huenda tukawa hatuna matumizi nazo au soko la kuziuza au ubebaji wake zikishanyofolewa mle ndani ni kazi ngumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo suala la msingi ni kwamba wataalamu waangie, kama uamuzi unaweza kufanyika ili kwa mara ya kwanza baada ya miaka hamsini hiyo bidhaa tunayosema chuma iweze kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wasukuma mtu akija kununua mpunga kwao, unachouliza kitu cha kwanza ni bei ya mchele, ukijua bei ya mchele ndipo unajua kwamba niuze mchele au niuze mpunga; lakini utaangalia gharama zako, waste na nini, ndiyo utatoa bei ya mpunga. Kwa hiyo hata hili nafikiri wataalamu wajaribu kufanya vice versa waone kama mtu anataka chuma waangalie bei ya gharama zao na waangalie bei ya waste na nini ili waamue kama wanaweza kuuza ni vizuri Serikali ikauza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna hili tatizo la bidhaa ya mazao mbalimbali. Nimesikia wachangiaji, Waheshimiwa Wabunge hapa wameongea sana suala la mihogo kwenda kutafuta wateja China, kufanya nini; lakini mimi nilikuja hapa na wazo na kwenye Kamati tulijaribu kuliongea na kuliingiza. Lugha niliyotumia ilileta mtafaruku kidogo niliposema kwamba wananchi waruhusiwe kutengeneza gongo kutokana na mahindi, muhogo na mtama. Maana yangu, gongo ni kama kusema kitimoto kwenye nguruwe, lakini maana yangu ni spirit. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, gongo ni neno la mtaani kama vile kitimoto, lakini maana yake ni spirit. Pombe zote kali tunazokunywa hapa ni spirit. Hata tukiwauzia Wachina mahindi au muhogo, wakatengeneza spirit ile ile wataturudishia sisi. Kwa hiyo, sasa hivi sisi tunachokunywa ni spirit kutoka kwenye mahindi ya watu wa nje. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Sawa sawa.

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna ubaya gani Serikali isiruhusu gongo, iruhusu spirit itengenezwe. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, iruhusu spirit kutoka kwenye mazao ya chakula ili iweze kusaidia na kuinua bei ya mazao. Najua kuna wachangiaji wengi kwenye mtandao wanajaribu kusema kwamba bei ya vyakula itapanda, lakini leo hatuna njaa ya chakula, njaa yetu kubwa ni pesa. Maana yake vyakula vimebadilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mchele, leo tuna competition kubwa sana ya chips. Tunalia sana mikoa inayozalisha mchele, maana yake watu wameanza kula viazi vitamu ambavyo ni chips. Na sisi watu wa Mwanza na Shinyanga hatuwezi kulalamika kwa kuwa watu wameanza kula chips, ni pamoja na sisi wenyewe; na bahati nzuri watoto wameipenda chips. Sasa sisi wenye mchele tutafanya nini? Ni lazima tutafute option nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri wataalam wetu wajaribu ku-review kidogo mawazo, itatusaidia sana. Maana yake elimu tunayotumia imeandikwa zaidi ya miaka 50 na dunia inakwenda haraka: Je, wataalam wanajaribu kweli ku- review mawazo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najaribu kumalizia kwa kuongea, suala hili limetusumbua sana hasa kwenye Kamati yetu ya Madini tulivyokuwa juzi kwenye kikao. Mheshimiwa Rais ame-invest pesa nyingi sana kwenye ndege zaidi ya shilingi trilioni moja. Ndege hizo tunatarajia ziende nje zikalete watalii na watalii watuletee dola. Hata hivyo, dola sisi hatui- charge tax, lakini dhahabu tunai-charge tax na dhahabu ni currency. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Ni fedha!

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, dhahabu ni pesa na ni pesa ya kwanza kabla ya pesa hizi tunazozitumia za karatasi. Nafikiri kwa nyie wenzetu wasomi mnaelewa, pesa ya kwanza duniani ni dhahabu, lakini kwa nini tutumie gharama ya shilingi trilioni moja kufuata dola kwa Mchina Uchina? Tunakataa currency ya mtu ambaye hana viatu wala kitu chochote, hajaomba huduma ya Serikali, anatuletea dhahabu; na leo tunalia na Mheshimiwa Mpango, tuna deficit ya dola; lakini dola zipo mlangoni na watu walionazo hawana tatizo lolote. Tunataka tax ya nini? Mbona dola hatui-charge tax? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda na dola kwenye benki, unachoulizwa zaidi ni kwamba unazo nyingi tukuongeze bei? Mbona huyu wa dhahabu haambiwi kwamba unazo tukuongeze bei? Badala yake anaambiwa tutakukata. Ukimwambia utamkata, anakataa. (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana wataalam wetu wajaribu sana ku-review, maana yake elimu wanayotumia, hatukatai, lakini elimu isiwe kama Biblia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi hata Baba Mtakatifu anafanya marekebisho kwenye Kanisa Katoliki ili kusudi Kanisa lisiwe gumu na Walokole wasimalize wafuasi. Maana yake kwa ajili ya ugumu ule, Walokole wameendelea kuchukua wafuasi. Kwa hiyo, tunaomba na ndugu zetu; Mheshimiwa Mpango, jaribu kidogo kuchukua na elimu ya Mtaani ili ijaribu kutuinua kwenye uchumi. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)