Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Kiteto Zawadi Koshuma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuendelea kutoa michango yangu katika Bunge lako hili Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nianze kwa utangulizi ufuatao. Sasa tunaelekea mwisho wa miaka mitano ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa 2016 - 2021 na sasa tuko katika Mpango wa Nne ambao ndiyo tuko tunaujadili sasa hivi. Naomba wakati tunajadili Mpango huu wa Nne wa Maendeleo ya Taifa, naomba tuangalie baadhi ya mambo ambayo kama itapendeza Wizara kama walivyoahidi katika kitabu chao kwamba wanachukua maoni yetu kwa sababu haya ni Mapendekezo ya Mpango, kwa hiyo, kama itawapendeza kuchukua mawazo yangu basi nitashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuanza kwa kuangalia hali ya uchumi katika Taifa hili la Tanzania. Hali ya uchumi katika Taifa hili la Tanzania kutokana na taarifa ya Mheshimiwa Waziri, anasema kwamba hali ya uchumi imeimarika. Hata hivyo, ukiangalia hali ya uchumi wa mwananchi mmoja mmoja bado ni duni, purchasing na buying power ya wananchi imepungua na iko chini sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwananchi wa hali ya kawaida kwa sasa hivi, kwanza kabisa vifaa vya ujenzi vimepanda bei kiasi kwamba mwananchi tu wa kawaida hata kujenga nyumba inamuwia vigumu. Ukiangalia katika zile basic needs, nyumba ni kitu cha msingi sana lakini maisha ya mwananchi bado yako duni kiasi kwamba hawezi kuwa na uwezo wa kujenga nyumba kwa sababu vifaa vya ujenzi vimepanda bei. Hata katika taarifa ya Mheshimiwa Waziri ameeleza kwamba mfumuko wa bei kwa sasa hivi umepungua. Ni kweli katika vitu vidogo vidogo kama vile vyakula lakini masuala yale ya msingi ambayo yanaweza kusaidia mwananchi kuwa na maendeleo hali bado sio nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia vilevile wakati uchumi wa Taifa wenyewe unakua lakini uchumi wa wananchi unaendelea kuwa duni, bado wapo wezi, mimi nawaita wezi. Kumezuka janga kwa hawa watu wenye hizi betting centers, nitazitaja, sasa hivi kuna Tatu Mzuka, Premier Bet, Moja Bet na Biko, hawa wote ni wezi ambao wanaiba fedha za wananchi katika mifuko yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nasema hawa ni wezi kwa sababu hiki wanachokifanya ni sawasawa na upatu. Sisi wenyewe wananchi ndiyo tunatoa pesa zetu halafu baadaye wanatokea wanatangaza kwamba kuna mshindi ameshinda shilingi milioni 100. Hata hivyo, ukiangalia wananchi ndiyo wame-contribute zile fedha, zimefika shilingi bilioni moja huyu mtu amekusanya, kwa kuwa yeye hana mtaji, halafu mwisho wa siku sasa, wananchi kwenye mifuko yao wanabaki bila fedha, halafu anatokea mtu mmoja anatangazwa mshindi anachukua shilingi milioni 100 yeye katajirika. Huu ni wizi wa waziwazi kabisa, mimi nimeangalia nimeona hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba kuishauri Serikali kwamba sasa tunapojadili Mpango huu wa Nne hebu tuangalie tunasaidiaje wananchi kutoka katika hali ya umaskini ili waweze kujikomboa na kuwa na maisha mazuri. Kwa sababu hauwezi ukajinadi ukasema kwamba uchumi wa nchi unakua wakati hali ya wananchi wako inazidi kuwa duni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naishauri Serikali kama ikipendeza wachukue maoni haya, waweke mkakati wa kuhakikisha wanazi-control hizi betting centers, waangalie ni kwa namna gani hizi betting centers...

T A A R I F A . . .

MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namheshimu sana mdogo wangu Mheshimiwa Salome na naamini kabisa ame-scrutinize kitu ambacho amekisema kabla hajanipa taarifa hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, japokuwa hawa watu wa betting centers wapo kisheria lakini mimi naangalia ni namna gani wanaiba fedha katika mifuko ya wananchi. Ndiyo maana naendelea kuishauri Serikali iangalie ni namna gani wanaweza kuzi-control hizi betting centers ili wasiendelee kuchukua fedha katika mifuko ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimeshaishauri Serikali iangalie controlling ya hizo betting centers.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kutokana na hali ya wananchi wetu kuendelea kuwa duni, solution mojawapo ambayo Serikali inaweza kuifanya ni kuongeza Government expenditure. Serikali ijitahidi katika kuhakikisha kwamba inatumia sana ili kule chini mzunguko wa fedha uendelee kuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia ambapo sasa tunaenda katika Mpango huu wa Nne, ukiangalia fedha za maendeleo katika Halmashauri zetu haziendi. Waheshimiwa Wabunge wataniunga mkono kwa sababu wamekuwa wakisema mara kwa mara humu ndani kwamba fedha za maendeleo katika Halmashauri zetu haziendi, ni sifuri kabisa. Sasa unategemea ni kwa namna gani hawa wananchi wanaweza wakawa na maendeleo wakati fedha za maendeleo kwenye Halmashauri haziendi, ina maana kule kwenye Halmashauri zetu hakuna miradi yoyote ambayo inaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ukiangalia katika kitabu cha Mheshimiwa Waziri katika changamoto ambazo amezisema, amesema changamoto mojawapo ni kutokuweza kuwalipa wakandarasi wa ndani pamoja na wazabuni mbalimbali. Nashauri Serikali basi iweze kuweka mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba wakandarasi na hawa wazabuni wanalipwa kwa wakati ili wananchi waweze kuwa na mzunguko wa fedha waweze kujikimu kimaisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nionglee suala la deni la Taifa. Mara kwa mara nimekuwa nikiongelea suala la deni la Taifa na leo sitaweza kuliongelea kwa muda mrefu kwa sababu ya muda kutoniruhusu. Deni la Taifa tunaliona linaendelea kuongezeka. Kwa taarifa ambazo siyo rasmi, deni letu la Taifa sasa limeongezeka kwa asilimia 46.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sipingani kwamba tusikope, tukope lakini lazima tuweke mikakati madhubuti ya kuhakikisha kwamba tunaweka control ya ukomo wa deni. Tusiwe tunakaa tunasema kwamba deni letu ni stahimilivu na hivyo tuendelee tu kukopa pasipokuwa na mpango mkakati wa ukomo wa kukopa, tutakopa mpaka shilingi ngapi na tunavyozikopa hizo fedha tutazikopa kwa sababu ya nini? Ningefurahi sana tunapotengeneza Mpango huu wa Nne tuangalie ni kwa namna gani tunali-control deni letu la Taifa ili lisiendelee kuwa kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia sasa hivi karibia asilimia 35 ya mapato ya ndani inatumika kulipa deni la Taifa. Hii inasababisha baadhi ya miradi kuzorota na kutoweza kukamilika kwa wakati. Kwa hiyo, nashauri Serikali iangalie namna gani ya kuweza kuli-control deni hili la Taifa ili tusije tukajikuta tunaingia katika nchi ambazo na zenyewe zimeingia katika debt stress, zimepata stress ya madeni. Ukiangalia nchi kama Mozambique wamekuwa wakikopa na kukopa, Serikali inakuwa inasema kwamba deni ni stahimilivu hatimaye sasa hivi Mozambique imeletewa kuwa ni nchi ambayo imeingia katika debt stress. Sitapenda Serikali ya Tanzania au nchi ya Tanzania iingie katika kuwa na debt stress. Kwa hiyo, nashauri Serikali iweke good management ya deni letu la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kama muda wangu unaruhusu, naomba Serikali iweke mkakati wa kuwakikisha kwamba wanaachana na suala la kukopa mikopo ambayo ina riba kubwa, wakope mikopo yenye riba nafuu ili tuweze kuwa na uwezo wa services deni letu. Kwa maana kwamba tukifanya hivyo, basi tunaweza kuchochea maendeleo ya wananchi katika nchi ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala lingine naomba kushauri Serikali ijitahidi kuwawezesha wataalam kupata mafunzo ya negotiation skills ili wanapoenda kujadili mikataba ya kukopa haya madeni ya Taifa waangalie zile contract ambazo wanaweka kwamba zina manufaa gani katika nchi yetu. Sasa hivi China amekuwa anakopesha nchi za Afrika na China ni mjanja sana anamkopesha mpaka Mmarekani lakini anapokuja kuzikopesha nchi za Afrika anajuwa sisi hatuna negotiation skills, kwa hiyo, yeye analeta masharti yake na sisi tunayakubali wakati yale masharti yanakuwa siyo mazuri. Unakuta Mchina anakukopesha halafu anakwambia wafanyakazi wake ndiyo wafanye kazi wakati sisi wananchi wetu wapo na wana uwezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti naiomba Serikali iweze kuangalia wanapokwenda kujadili mikataba ya kimataifa kuhusu mikopo wajue wanakopa kwa ajili gani, kwa sababu gani na mikopo ya bei nafuu. Nashukuru sana naunga mkono hoja.