United Republic of Tanzania
Parliament of Tanzania
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa amempongeza Spika wa Bunge Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson kwa kubuni na kulitekeleza Bonanza la kimichezo la Bunge ambalo limeanza kufanyika leo tarehe 28 Janauari, 2023 Jijini Dodoma.
Akizungumza
wakati wa Bonanza hilo, Waziri Mkuu ambaye ndiye alikuwa Mgeni rasmi amesema
kuwa bonanza hilo limefana sana na kama
kuna mapungufu ni kidogo ambayo hata hivyo yatafanyiwa kazi ili bonanza lijalo
liwe bora zaidi.
“Nakupongeza
sana Mheshimiwa Spika kwa kubuni wazo la kuwa na bonanza na kulitekeleza.
Limefana sana na kwa kuwa ndio linaanza naamini Bonanza lijalo litakuwa bora
zaidi,” alisema Waziri Mkuu.
Aidha Waziri Mkuu amewaasa Waheshimiwa Wabunge
na Watumishi wa Ofisi ya Bunge kutumia bonanza kama sehemu ya kufanyia mazoezi
kwa ajili ya kuimarisha afya ya miili yao.
“Tunatumia
muda mwingi sana kukaa wakati tunatekeleza majukumu yetu, hivyo mazoezi ya Bonanza
hili yatatuweka timamu kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yetu,” alisema.
Waziri Mkuu aliongeza pia kuwa
mbali na mazoezi bonanza hilo lina faida nyingine zikiwemo kujenga urafiki na
kudumisha udugu miongoni mwa washiriki.
“Faida
nyingine ya bonanza hili ni kukuza vipaji vya kucheza michezo mingi kwa kuwa
bonanza hili linahusisha michezo mingi ambayo inatoa fursa kwa kila mmoja
kushiriki,” alisema.
Kwa
upande mwingine, Waziri Mkuu aliwashukuru pia wadau mbalimbali ambao
walifanikisha kufanyika kwa tamasha hilo wakiwemo Benki ya NMB ambao ndio
walikuwa wadhamini wakuu wa bonanza la siku ya leo.
Awali
akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa bonanza hilo, Spika wa
Bunge Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson aliwashukuru na kuwapongeza wote
walioshiriki katika tamasha hilo.
Aidha
alisema bonanza hilo limeanza vizuri na kwamba changamoto ndogo ndogo
zilijitokeza zitafanyiwa kazi kwa ajili ya kufanikisha mabonanza bora zaidi.
“Bonanza
hili limeonesha ya kwamba tuna uwezo wa kufanya mazoezi na pia kuwahamasisha
wanananchi kufanya hivyo,” alisema.
Mbali na
Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watumishi wa
Bunge, bonanza la leo pia lilihusisha wawakilishi kutoka Baraza la Wawakilishi
Zanzibar.
Bonanza
la Bunge la kimichezo la leo lilihusisha michezo takribani 19 ambapo kwa kiasi
kikubwa Waheshimiwa Wabunge waliibuka
washindi katika michezo hiyo na hivyo kuchukua vikombe vingi pamoja na Kombe la
ushindi ambalo Mwenyekiti wa Bunge Bonanza Mheshimiwa Festo Sanga alikabidhiwa na Waziri Mkuu.
Bonanza
hilo limepangwa kufanyika mara nne kwa
mwaka ambapo bonanza lijalo linatarajiwa kufanyika tarehe 24 Juni, 2023. Kauli Mbiu ya
Bonanza la leo ilikuwa: Shiriki Michezo Tujenge Taifa Lenye Afya.