Parliament of Tanzania

WAGOMBEA WALIOPITISHWA NA VYAMA VYA SIASA KUGOMBEA NAFASI YA USPIKA

Jumla ya wagombea nane (8) wamejitokeza kugombea kiti cha Spika wa Bunge la Kumi na Moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akiongea na waandishi wa habari leo mjini Dodoma, Katibu wa Bunge, Dkt Thomas Kashilillah amesema, “nimepokea majina nane kutoka vyama nane vya siasa watakaogombea nafasi ya Spika wa Bunge la Kumi na Moja la Jamhuri ya Muungano .”

Amewataja waliojitokeza kuwania nafasi hiyo kuwa ni, Mhe. Peter Leonard Sarungi kutoka chama cha Alliance for Tanzania Party (AFP), Mhe. Hassan Kisabya Almas kutoka Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA), Mhe. Dkt. Godfrey Rafael Malisa kutoka Chama cha Kijamii (CCK), na Mhe. Job Yustino Ndugai (Mb) kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM).

Wengine ni Mhe. Goodluck Joseph Ole Medeye kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mhe. Richard Shedrack Lyimo kutoka Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Mhe. Hashim Spunda Rungwe kutoka CHAUMMA na Mhe. Robert Alexander Kasinini, Chama cha Democratic Party (DP).

Kwa mujibu wa Dkt Kashilillah, uchaguzi wa Spika utafanyika kesho tarehe 17 Novemba, 2015 kuanzia saa tatu asubuhi katika ukumbi wa Bunge mjini Dodoma.

Mbali na kutaja majina ya wagombea wa Spika wa Bunge, Dkt Kashilillah amesema mpaka tarehe 16/11/2015 jumla ya wabunge 348 wamekwisha sajiliwa.

Aidha Dkt Kashilillah amesema kuwa maandalizi yote kwa ajili ya mkutano wa 11 wa bunge yamekamilika.

Katika mkutano huo wa kwanza wa bunge la 11, kutakuwa na shughuli mbalimbali zikiwemo kumchagua Spika, Naibu Spika na kuthibitisha jina la Waziri Mkuu.

Ms. Nenelwa J. Mwihambi

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's