United Republic of Tanzania
Parliament of Tanzania
MAELEZO MAFUPI YA KAIMU KATIBU WA BUNGE KWA
WAANDISHI WA HABARI KUHUSU WITO WA WABUNGE
WATEULE NA ZOEZI LA USAJILI.
_________________
DAR ES SALAAM,
1 NOVEMBA, 2015
Ndugu Wanahabari,
Naomba kuchukua nafasi hii kuwapongezeni kwa kazi yenu nzuri na kubwa ya kuuhabarisha umma hususani katika kipindi hiki chote tulichopitia cha zoezi muhimu la Uchaguizi Mkuu wa Mwaka 2015 hadi kufikia leo uchaguzi umekwisha na tayari watanzania wamekwisha kufanya maamuzi ya kuchagua viongozi wao kuanzia ngazi ya Rais, Wabunge na Madiwani.
Nimewaita hapa kuzungumzia baadhi ya mambo yanayofuata baada ya kumalizika kwa uchaguzi hususani baada ya kupatikana kwa Wabunge wateule majimboni.
Ni dhahiri kuwa, kufuatia kumalizika kwa uchaguzi Mkuu, Wananchi na Wabunge wengie wateule wangependa kufahamu hatua inayofuata kwa upande wa Bunge.
Napenda kuwatangazia Wabunge wateule wote walioko majimboni kuwa, wanatakiwa kuwasili jijini Dar es salaam kuanzia jumatano tarehe 4 Novemba, 2015 ili waweze kushiriki hafla ya kuapishwa kwa Rais Mteule itakayofanyika tarehe 5 Novemba, 2015 katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.
MAMBO YA KUZINGATIA KWA WABUNGE WATEULE KABLA YA KUFIKA DAR ES SALAAM
Kabla ya kusafiri kuja Dar es Salaam kwa Wabunge wote Wateule, ni lazima wawe wamepatiwa cheti cha Kuteuliwa kuwa Mbunge kinachotolewa na Msimamizi wa uchaguzi ambacho baada ya zoezi la kuapishwa kwa Rais Mteule, zoezi litakalofuata ni Usajili wa Wabunge hao wateule.
Kila Mbunge Mteule atatakiwa kuwasilisha cheti hicho kwa Maafisa wa Bunge wakati wa Zoezi la Usajili. Aidha pamoja na cheti hicho, kila Mbunge Mteule anatakiwa kuja na kitambulisho kingine chochote kinachotolewa na mamlaka inayotambulika na kinachomtambulisha jina lake kamili kama linavyooneka kwenye cheti cha Kuteuliwa kuwa Mbunge.
Matarajio ni kwamba, zoezi la usajili kwa Wabunge wote wateule litafanyika katika viwanja vwa Bunge Mjini Dodoma. Hivyo basi wabunge wote wateule watatakiwa kujitegemea katika usafiri kuelekea Bungeni Dodoma tayari kwa kuanza kwa zoezi hilo kabla ya Mkutano wa kwanza wa Bunge la Kumi na Moja.
Ndugu wanahabari,
Mkutano wa kwanza wa Bunge la kumi na Moja unatarajiwa kuanza siku ambayo Rais atahitisha Bunge. Ratiba kamili itatolewa baadae na shughuli zitakazofanywa katika Mkutano wa kwanza zitahusisha:
· Uchaguzi na Kiapo kwa Mhe. Spika
· Viapo kwa Wabunge wote
· Kuthibitisho wa Jina la Waziri Mkuu
· Uchaguzi wa Naibu Spika
· Ufunguzi Rasmi wa Bunge la Kumi na Moja
Ndugu wanahabari,
Naomba nivikumbushe, vyama vyote vya Siasa vyenye usajili wa kudumu na ambavyo vina nia ya kusimamisha mgombea wa nafasi ya Spika kuwa vinatakiwa kuanza mchakato wa kumpata mgombea wa nafasi hiyo katika ngazi ya vyama ili baada ya tangazo la nafasi ya Spika kuwa wazi, viwe vimekamilisha mchakato huo kwa kuwasilisha jina la Mgombea kwa Katibu wa Bunge.
Vyama vya siasa hivyo havina budi kuzingatia kuwa mgombea wa nafasi ya Spika anaweza kuwa Mbunge au mwanachama yeyote wa chama hicho kwa masharti kwamba kama sio Mbunge mteule, jina lake lazima liwasilishwe kwanza Tume ya Uchaguzi siku tano kabla ya uchaguzi kujiridhisha kwamba mgombea huyo ana sifa za kuwa Mbunge.
Kwa maelezo haya mafupi, nimatumaini yangu mtatumia nafasi hii kuwafahamisha Wabunge wote wateule na Wananchi kwa Ujumla kuhusu shughuli yetu hii kubwa iliyoko mbele yetu tayari kwa kuanza kwa Bunge la Kumi na Moja.
Asanteni sana kwa Kunisikiliza,
John Joel
KAIMU KATIBU WA BUNGE