United Republic of Tanzania
Parliament of Tanzania
Wakati Kamati za Kudumu za Bunge zikiwa zimeanza shughuli zake Mjini Dodoma ikiwa ni siku chache kabla ya kuanza Mkutano wa Bunge unaotarajiwa kuanza tarehe 6 Septemba, MKURUGENZI wa Halmashauri ya Gairo, Agnes Mkandya, amejikuta akibubujika machozi mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za serikali za Mitaa(LAAC) wakati akijibu hoja za wajumbe, akidai Halmashauri hiyo ni chafu kwa vitendo vya ubadhirifu wa fedha.
Hali hiyo ilijitokeza wakati akihojiwa na Kamati ya LAAC ambayo iliongozwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye ni Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Vedasto Ngombale(CUF),kutokana na hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) za mwaka 2013/14.
Mkurugenzi huyo alitokwa na machozi wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti maalum, Leah Komanya(CCM) aliyetaka kujua pamoja na Halmashauri hiyo kuwa na sera ya kukabiliana na vitendo vya ubadhirifu wa fedha lakini imejipangaje kwa kuwa wana ubadhirifu upande wa uhasibu.
Kadhalika, alimtaka Mkurugenzi aeleze ni kwa nini Halmashauri imekuwa ikishindwa kujipanga katika kusimamia mapato na ina mpango gani wa kuunganisha mfumo wa udhitibiti wa ndani.
“Pamoja na uwepo wa ubadhirifu kwa upande wa uhasibu si kwenye mapato tu bali hata matumizi ya mfumo mzima wa "EPICOR" ubadhirifu huu unatokana na Halmashauri haijafunga mfumo wa kieletroniki,”alisema Komanya
Alisema kutokana na kutotumia mfumo huo ndio sababu ya ubadhirifu wa fedha unaofanywa na watendaji kwa kughushi stakabadhi ambapo anapokea sh. 5000 lakini anaandika kwenye stakabadhi sh. 3000.
Sambamba na hilo, Wajumbe wa LAAC walitaka kujua sababu za fedha za kwaajili ya Wanawake na Vijana kutokwenda kwenye vikundi wakati zilikuwa zimetengwa kiasi cha sh. milioni 30 kwa mwaka huo lakini zilizopelekwa ni sh. Milioni tatu.
Kadhalika, kulikuwa na hoja ya kiasi cha sh. milioni 24.3 kwa ajili ya kwenda kwenye vijiji na mitaa hazijapelekwa.
Akijibu hoja hizo, Mkurugenzi akijikuta akishindwa kumalizia kujibu hoja hizo na akiangua kilio huku akisema mashine 20 za mfumo wa kielektroniki tayari zimenunuliwa na wanasubiri kampuni ya simu ya TTCL kufunga mfumo huo.
Aidha alisema jumla ya wakuu wa idara tisa katika halmashauri hiyo wamesimamishwa kazi, kutokana na ubadhirifu hali iliyomfanya ashindwe kumaliza kutoa maelezo na kuanza kulia akidai halmashauri hiyo ni chafu mno.
Mkurugenzi huyo alisema licha ya kuwa ni mgeni katika halmashauri hiyo alikuta halmashauri hiyo ikiwa na uchafu mkubwa kutokana na kuwepo kwa watumishi wabadhirifu.
Kuhusu fedha za mfuko wa wanawake na vijana, alikiri fedha hizo kutopelekwa na kwamba wamejipanga katika kipindi cha miezi nane hadi machi 2017 kulipa fedha hizo kwa kutumia mapato yake.
Kufuatia kutoridhishwa na majibu ya halmashauri hiyo, Kamati hiyo iliagiza halmashauri ya wilaya ya Gairo kulipa deni la mfuko wa maendeleo ya wanawake na vijana la sh. milioni 27.9 la mwaka 2013/2014 ndani ya kipindi cha miezi sita kuanzia sasa.
Mbali na hilo pia LAAC iliagiza halmashauri ya Kilosa kuilipa halmashauri ya Gairo sh. milioni 24.3 ndani ya miezi sita fedha ambazo zilikuwa kwa ajili ya kwenda kwenye vijiji na mitaa.
Akitoa maagizo hayo, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Abdallah Chikota, alisema deni la mfuko wa maendeleo ya wanawake ni sh. milioni 13.4 na mfuko wa maendeleo ya vijana ni sh. milioni 14.4.
Alisema kutokana na maagizo hayo mwenyekiti na mkurugenzi wa halmashauri ya Gairo wanapaswa kuandika barua ya kuthibitisha ulipaji wa deni hilo na kuiwasilisha kwa sekretarieti kabla ya agosti 23 mwaka huu lakini pia kupitia vikao vya kinidhamu kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi waliobainika kuhusika na ubadhirifu ndani ya halmashauri.
Alisema kamati inaiagiza ofisi ya rais tawala za mikoa na serikali za mitaa(TAMISEMI) na ofisi ya katibu tawala wa mkoa(RAS) mkoa wa Morogoro kusimamia kwa ukaribu utendaji kazi wa halmashauri ya wilaya ya Gairo.
Hata hivyo aliitaka TAMISEMI kuhakikisha deni lote la halmashauri ya Gairo la sh. milioni 254 kutoka halmashauri ya wilaya ya Kilosa linalipwa katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 ambalo lilitokana fedha hizo kuingia katika halmashauri hiyo kutokana na Gairo kuwa halmashauri mpya na hivyo kutokuwa na akaunti kwa kipindi hicho.