United Republic of Tanzania
Parliament of Tanzania
SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amesema Bunge la Tanzania linatarajia kuwa na uhusiano wa kudumu na Bunge la Sweden.
Spika alisema hayo jana wakati akizungumza na ujumbe wa wabunge kutoka Nchini Sweden walipotembelea Ofisi Ndogo za Bunge Jijini Dar es Salaam.
Alisema Tanzania na Bunge kwa ujumla imepata bahari kutembelewa na wabunge hao ambao pia wamekuja kufuatilia namna ambavyo nchi yao inashirikiana na Tanzania.
“Vilevile ujumbe wa wabunge hawa umekuja kuhakikisha wanajenga uhusiano wa kibunge na ni hakika ugeni wao utaimarisha uhusiano wa Bunge letu na lao.
“Wabunge wetu pamoja na wafanyakazi watapata fursa ya kwenda Sweden kuona jinsi Bunge la Sweden linavyofanya kazi lakini pia wabunge wa Sweden na wafanyakazi wenu mtapata fursa ya kutembelea Bunge letu,” alisema.
Mhe. Ndugai alisema uhusiano wa Tanzania na Sweden ni wa kihistoria tangu enzi za Hayati Mwalimu Julias Nyerere na aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Olof Palme na kwamba nchi hiyo ilisaidia pia ukombozi katika nchi za Afrika.
Aidha, alisema anatambua mchango wa Sweden katika kuisadia Tanzania kwenye sekta mbalimbali kama vile afya elimu na teknolojia ya gesi.
Kwa upande wake Balozi wa Sweden nchini, Katarina Rangnitt alisema yeye amewahi kupata nafasi ya kutembelea Bunge la Tanzania na kushuhudia jinsi linavyoendesha kwa demokrasia na uwazi.
Naye kiongozi wa msafara wa wabunge hao,Kenneth Forslund aliushukuru uongozi wa Bunge kwa mapokezi mazuri na kuahidi kuendeleza uhusiano wenye tija kati ya Bunge la Tanzania na Sweden.
Katika kikao hicho Mh. Spika alipata fursa ya kuelezea muundo wa Bunge la Tanzania pamoja na kujibu hoja mbalimbali za wabunge hao kutoka Sweden.
Ugeni huo pia ulipata fursa ya kukutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na kuzungumza masuala mbalimbali yanayohusu uhusiano wa nchi hizo mbili ikiwemo uhusiano wa kibiashara.