United Republic of Tanzania
Parliament of Tanzania
Waheshimiwa Wabunge,
Tunaendelea kuomboleza msiba wa mpendwa wetu Marehemu Mzee Samuel John Sitta, Spika Mstaafu wa Bunge la Tisa uliotokea usiku wa kuamkia jana huko Munich, Ujerumani.
Mazishi ya Spika Mstaafu yako kwa mujibu wa Sheria ya Mazishi ya Viongozi ya Mwaka 2006 ambapo Serikali ndio inayoratibu taratibu zote za mazishi hayo. Hivyo, tunaendelea kuwasiliana na wenzetu Serikalini juu ya taratibu za mazishi hayo pamoja na namna Bunge letu linavyoweza kushiriki kumuaga marehemu mpendwa wetu Mzee Samuel Sitta.
Jana Tume ya Utumishi wa Bunge ilikaa na kuandaa taratibu mbalimbali za namna Bunge letu litakavyoshiriki na leo hii nimetuma Maafisa Dar es Salaam kwenda kuungana na wenzetu Serikalini katika kuratibu mazishi hayo.
Kama mnavyofahamu, Ofisi ya Bunge ilikuwa ikigharamia matibabu yake kuanzia Nchini India baadaye Uingereza na hatimaye Ujerumani ambako mauti yamemkuta, na hivyo Ofisi ya Bunge ndio inayogharamia usafirishaji wa mwili wake kutoka Ujerumani kuja nchini.
Mwili huo unatarajiwa kuondoka leo nchini Ujerumani kuja Tanzania na baada ya vikao vinavyoendelea Serikalini tutajulishana namna ya ushiriki wetu.
Lengo letu ni mwili huo kuweza kuletwa hapa Bungeni ili Waheshimiwa Wabunge wote mpate fursa ya kumuaga. Tutaendelelea kujulishana taratibu nyingine.
Job Y. Ndugai, Mb.
SPIKA
8 Novemba, 2016