United Republic of Tanzania
Parliament of Tanzania

SPIKA wa Bunge Mhe. Job Ndugai amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam, Mhe. Truong Tan Sang leo katika Hoteli ya Kilimanjaro 10 Machi, Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi habari muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo Rais huyo Mhe Ndugai amesema Bunge la Tanzania litaendelea kukuza ushirikiano na Bunge la Vietnam hiyo ikiwa ni kuendeleza uhusiano ulipo baina ya mataifa hayo mawili kwa kipindi cha miaka mingi.
Amesema Tanzania imekuwa na uhusiano mzuri na Vietnam ambapo mwaka 2009 Wabunge wa Tanzania walitembelea Bunge la Vietnam ambapo mwaka 2011 wabunge wa nchi hiyo nao walitembelea Bunge la Tanzania na kufanikiwa kubadilisha uzoefu wa Mabunge yao.
Spika wa Bunge amesema kupitia uongozi wake atahakikisha kuwa uhusiano huo wa bunge la Tanzania unakuwa endelevu kwa faida ya Tanzania na Watanaznia ambao wanawakilishwa na wabunge wao katika bunge.
Katika mazungumzo hayo Spika aliongozana na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti Hawa Ghasia, Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji Mhe. Mary Nagu na Mbunge wa Segerea na Wabunge wengine ambao ni Wajumbe wa Kamati mbalimbali.