United Republic of Tanzania
Parliament of Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli ameipongeza ofisi ya Bunge kwa kubana matumizi na kufanikiwa kuokoa shilingi Bilioni 6, ambazo zitatumika kutengeneza madawati ya wanafunzi wa shule na amezitaka ofisi na taasisi nyingine za serikali kuiga mfano huo.
Ameagiza fedha hizo zipelekwe Idara ya Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili vyombo hivyo vifanye kazi ya kutengeneza madawati yanayotarajiwa kuwa zaidi ya 120,000 ambayo yatasambazwa katika shule ili kukabiliana na tatizo la wanafunzi wanaokaa chini kwa kukosa madawati.
Hundi Kifani ya fedha hizo imekabidhiwa kwa Mheshimiwa Rais na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Akson, ambaye amesema Ofisi ya Bunge imetekeleza wito wa serikali wa kubana matumizi ambapo kiasi hicho cha shilingi Bilioni 6 kimepatikana kwa kipindi kifupi cha takribani nusu mwaka.
Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashilila ametaja maeneo ambayo Bunge limebana matumizi kuwa ni Safari za nje ya nchi, Mafunzo nje ya nchi, Machapisho na ununuzi wa majarida, Shajala, Chakula na Viburudisho, Mtandao, Malazi hotelini, Matibabu ya wabunge na familia zao nje ya nchi, Umeme, Maji, Simu na Uendeshaji wa Mitambo.
“Baada ya kufanyika kwa mapitio ya bajeti kwa kipindi cha nusu mwaka, tathmini hiyo iliwasilishwa kwa Spika wa Bunge, Mh. Job Ndugai ambaye alielekeza kiasi hicho cha fedha kilichosalia kitumike kwa ajili ya kupunguza tatizo la uhaba wa madawati kwa wanafunzi nchini,” alisema Katibu wa Bunge.