Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. John John Mnyika

Supplementary Questions
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Katika jibu la nyongeza imeelezwa kwamba ulipaji wa pensheni kwa wazee hawa utaanza kwa wazee ambao wana miaka kuanzia 70 wakati ambapo watu wanastaafu wengine wakiwa na miaka 55, wengine miaka 60 na umri wa kuishi Tanzania unajulikana. Je, Serikali hii ya CCM haioni kwamba inasubiri mpaka wazee wengi wafe ndiyo waweke mpango wa kuwalipa?
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwanza Mheshimiwa Naibu Waziri katika sehemu (a) ya swali hajajibu swali. Niliuliza ni lini hii fidia ya hisani italipwa lakini hajajibu ni lini na Mheshimiwa Lukuvi, Waziri wa Ardhi anafahamu kwamba jambo hili ni la muda mrefu. Mwaka 2009 aliyekuwa Waziri wa Ardhi wakati huo Chiligati aliahidi wangelipwa milioni tisa, hawakulipwa mpaka mwaka 2015 wananchi wakaandamana kwenda Wizarani, Serikali ikaahidi kulipa milioni mbili badala ya ile milioni tisa. Sasa sehemu (a) ni vyema Waziri akajibu ni lini hasa Serikali italipa hii fidia. Au inataka sasa kwa kuwa wakati ule tuliandamana kwenda Wizara ya Ardhi sasa tuandamane kwenda kwa Mheshimiwa Magufuli ajibu ni lini hasa hii fidia italipwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sehemu (b) ya swali. Serikali imesema kwamba haidaiwi mapunjo ya fidia ya maendelezo. Hili jibu la Serikali ni jibu la uongo. Mwezi Aprili mwaka 2014 tulikuwa pamoja na Rais Dkt. Jakaya Kikwete pale Mloganzila, jambo hili likajitokeza na Rais akataka vielelezo tukamkabidhi na sio Rais tu, Wizarani kuna nakala za fomu za watu ambao kimsingi walipunjwa fidia za maendelezo kinyume kabisa na thamani halisi ya mali zilizokuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sababu Serikali imejibu uongo hapa Bungeni; je, Serikali iko tayari kurudi kwenda kuchunguza malalamiko ambayo yako tayari Wizarani? Vielelezo vyote viko Wizarani na ikalipa fidia ya maendelezo pamoja na kujibu maswali kwa ukweli?
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Wakati
likijibiwa swali juu ya Msitu wa Nyuki, Serikali imeeleza kwamba inakusudia
kuendeleza msitu huu kuwa sehemu ya vivutio vya utalii Dar es Salaam. Kwa
miaka mingi Serikali imekuwa ikitoa ahadi juu ya kuugeuza msitu wa akiba wa
Pande (Pande Forest Reserve) kuwa kivutio cha utalii, ikafikia hatua mpaka
Serikali ikatangaza tenda.
Sasa kama msitu huu mpaka leo haujakamilika kuwa kivutio cha utalii ni
miujiza gani ambayo Serikali inayo ili kuharakisha kwamba haya mapori ya Dar es
Salaam yageuzwe kuwa sehemu za utalii na kuingiza kipato kwa Dar es Salaam
badala ya kuyaacha kama yalivyo na hatimaye kugeuka kuwa misitu ya mauaji
kama ilivyokuwa pori la akiba la Mabwepande.
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Katika majibu yake Mheshimiwa Naibu Waziri amesema mradi wa Ruvu Juu umekamilika na kwamba maeneo ya ndani ya kilometa 12 kutoka bomba kuu yanapata maji hivi sasa na ameyataja maeneo ya Kibamba, Mbezi, Msigani na kwingineko ambayo yako ndani ya Jimbo la Kibamba. Ukweli ni kwamba ule mradi haujakamilika, yapo maeneo ambayo yana mabomba ya Mchina ambayo maji bado hayatoki.
Mheshimiwa Spika, napenda Mheshimiwa Naibu Waziri ajibu ukweli, kwa maeneo ambayo yana mabomba ya maji lakini maji hayatoki mpaka sasa, ni lini maji yatatoka kama anavyosema mradi umekamilika? Je, yuko tayari baada ya hapa twende tukakague huo mradi anaosema umekamilika lakini maji hayatoki?
MHE. JOHN J. MNYIKA. Mheshimiwa Spika, nashukuru. Inasikitisha majibu yanatoka ya namna hii, hili suala ni la tangu mwaka 2012 kilipovunjwa kituo cha mabasi cha Ubungo; na mwezi Oktoba, mwaka 2014 aliyekuwa Rais, Mheshimiwa Jakaya Kikwete alitamka kwamba kituo kitaanza kujengwa na akatoa mpaka muda mfupi wa kukamilika kwa kituo, lakini majibu mpaka sasa mwaka 2017 yanakuja namna hii.
Sasa swali, ni lini hasa hiki kituo kitakamilika ili kuondoa msongamano ulioko Kituo cha Ubungo ambacho kimeshavunjwa na kiko kwenye hali mbaya?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kituo hiki kinajengwa pembeni ya barabara ya Morogoro, na siku chache zilizopita TANROADS wametoa notice kwa wananchi wote wanaoishi pembezoni ya barabara ya Morogoro mita 121 kutoka katikati ya barabara kila upande. Kuweza ndani ya siku 28 kubomoa majengo yao. Ndani ya siku 28 mita 121 pande zote mbili za barabara kutoka katikati ya barabara. Sasa kwa kuangalia umbali ambao TANROADS umeutaja ni wazi ubomoaji huu utahusu kituo cha sasa cha mabasi ya kawaida ya Mbezi kilichopo. Vilevile kama umbali ni huu wa mita 121 kutoka katikati ya barabara hata hiki kituo kipya kitaguswa.
Mheshimiwa Spika, swali langu kwa Serikali ama Waziri mwenyewe ama Wizara hii ya TAMISEMI ama Wizara ya Ujenzi ijibu; kwa sababu huu umbali utaingilia hiki kituo ni kwa nini Serikali isitengue hili Tangazo lilitolewa na TANROADS la siku 28 ili majadiliano kwanza yafanyike kuhusu huu upana wa barabara sababu ni upana mkubwa sana ambao hauko kwenye barabara yoyote Tanzania? Mita 121 pande zote mbili za barabara kutoka katikati, naomba majibu ya Serikali.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's