|
|
| Home »Contribution |
|
| |
 |
E-mail this to a friend |
 |
Printable version |
 |
N'hunga, Juma Suleiman[CCM]
Dole Constituency |
|
|
|
|
|
| 20 |
29 |
13 July 2010 |
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2010/2011 Wizara ya Fedha na Uchumi |
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba yetu sote naomba nichukue nafasi hii nimshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyetujalia leo tukiwa wazima na wenye afya njema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina tofauti na wenzangu wanaotangaza nia. Mimi ninatangaza nia ya kutokugombea. Kwenye Bunge lako hili, nimehudhuria Mikutano 100. Kwa maana hiyo, nimeishi katika Bunge hili kwa mfululizo kwa miaka 25. Kabla ya hapo, niliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya miaka minne, nimefanya kazi Ikulu mwaka mmoja. Karibu miaka thelathini na zaidi nimefanya kazi.
Namshukuru sana Mwenyezi Mungu, kwa hiari yangu bila kushawishiwa, naamua kung’atuka. Bila ya kusahau, niseme tu na ninyi wenzangu mliokuwepo ndani ya Ukumbi na wale ambao hampo katika Ukumbi, kila mmoja katika nia yake Mwenyezi Mungu amjalie, basi aishi zaidi ndani ya Bunge hili mara mbili ya mimi. Nitafurahi sana nikija, nikiwakuta wenyeji wangu ninaowafahamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikutakie kila la kheri wewe, umeingia kipindi chako cha pili, ni kijana mtiifu, nimekaa na wewe vizuri. Nakuombea kila la kheri na bila shaka utashinda. Namshukuru sana Mheshimiwa Spika wa Bunge letu la Jamhuri ya Muungano kwa kipindi chake hiki, ameleta mageuzi makubwa sana katika Bunge hili, Kanuni na vitu vingine vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii umeingia hapa umevaa joho, Spika wetu zamani alikuwa anavaa Mgolole. Ni vitu tofauti kabisa! Hayo ni maendeleo. Naibu Spika na Wenyeviti walikuwa hawana kitu maalum cha kuvaa. Leo Bunge letu kweli ni la viwango na ninategemea kama Mungu atajaalia Mheshimiwa Spika na yeye apite katika Jimbo lake kwa kishindo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Uingereza pale ukipata Uspika, Wabunge wengine wa vyama vingine hawaji katika Jimbo lako. Kwa hiyo, unapita bila ya kupingwa. Kwa sababu ukigombea na Spika pale Uingereza utakuwa huna mpango wa kupitisha hoja binafsi. Kwa maana hiyo, wana Kanuni yao hiyo kwamba ukishafikia Uspika, wewe unapitishwa tu. Sasa ningewaomba vyama vingine vya Upinzani, basi Mheshimiwa Spika kule akapite bila kupingwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, nianze kusema kwamba mimi naunga mkono hoja hii ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa asilimia mia moja. La kwanza ambalo nitalizungumzia ni suala la pensheni. Pensheni kwa wastaafu wetu, Watanzania wanafanya kazi vizuri sana. Wanaenziwa wakati wanafanya kazi. Lakini wanapostaafu hali zao zinakuwa dhalili sana, baadhi yao pensheni zao ni ndogo. Pensheni hazilipwi kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata leo hii ni mwezi wa saba huu, pengine ndiyo wakati wa kulipwa pensheni mwezi wa sita. Lakini mpaka leo kwa msimu huu bado wastaafu mwezi huu hawajalipwa. Nasikitika sana, lakini hivi vyombo vya pensheni ndivyo vinavyojenga Vyuo Vikuu. Vyuo Vikuu vyote vimejengwa na pesa za wastaafu, lakini wastaafu wenyewe wako hoi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kusema tu kwamba Serikali iwaangalie upya kwamba watu wanaostaafu waweze kuishi kwa kulipwa pensheni inayoweza kweli kuendeleza maisha yao, siyo kulipwa pensheni kama msaada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maneno mengine ni kwamba, nilipokuwa namsikiliza Mheshimiwa Waziri alisema kwamba kuna changamoto kwamba kila makisio yanapofanywa, basi huwa hayafikii kiwango. Hivi kwa nini makisio haya hayafikii kiwango, au makusanyo hayafikii kiwango? Kwa nini basi Serikali isingeangalia upya vyanzo vyetu viko namna gani? Viwango vyetu vya kodi viko sawa? TRA inafanya kazi vizuri? TISCAN ikoje? Kuna mwanya kiasi gani ambao unasababisha viwango visifikiwe?
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza ukashangaa sana, ukienda pale TRA ukaangalia hali halisi utashangaa kazi inavyokwenda. Makontena yanayokuja pale, urasimu uliokuwepo pale utaudhika!
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeiomba Serikali iangalie uwezekano wa kuondoa urasimu. Jambo lingine ambalo nitaliomba na lenyewe ni kuhusu suala la Bandari. Tanzania ni tajiri wa bandari. Mtwara kuna bandari, Lindi kuna bandari, Tanga kuna bandari, Dar es Salaam kuna bandari na Zanzibar kuna bandari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kwa nini bandari zote hizi, moja hatuteui ikawa bandari huru? Nimeambiwa hapa Pemba kuna bandari. Tuteue bandari moja iwe huru. Ukienda Singapore utakuta kuna bandari huru, wanapakia mizigo, wanashusha kwa wakati, haraka zaidi. Hong-Kong ukienda utakuta kuna bandari huru. Wanafanya kazi nzuri. Dubai wana bandari huru. Sisi kwa nini hili jambo hatulitilii maanani? Kwa mfano ukiweka bandari huru pale Zanzibar itakuwa ni bandari itakayohudumia Afrika ya Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii wakati mwingine unaona bora kushusha mzigo wako Mombasa kuliko kushusha Dar es Salaam kwa sababu gharama ni kubwa. Ukaushie Mombasa, uutoe Mombasa, uuingize Tanzania, bado gharama za kutoa kule kuuleta huku ni rahisi. Nini sababu? Urasimu! Ningemwomba Mheshimiwa Waziri hili aliangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nitakalolisemea ni la bidhaa feki. Tunaona bidhaa feki nyingi zinaingia katika nchi na kuvurugwa. Hivi nini kutufanyia uchuro katika nchi yetu ? Unaivuruga TV wewe mwenyewe kuitengeneza huwezi, unasema feki. Kwa nini bidhaa hizo zisikaguliwe huko huko zinakotoka? Vikaguliwe huko huko kama mtu kaenda kununua China, China huko huko. Maana watu wanaonunua magari Hong-Kong, Uingereza, TBS iko kule kule. TBS wanakwambia kwamba gari hii haiwezi kuingia Tanzania, haina sifa, huko huko! Unalipa dola 250 kila gari huko huko, ikifika hapa ina kibali cha TBS. Kwa nini basi watu wetu wa TBS hawa wa viwango vya hizo bidhaa wasiwe huko huko, vikafelishwa huko huko, vikarudi huko huko kuliko kutuingizia mzigo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba hilo na lenyewe liangaliwe. Pale bandari ninakumbushwa kuna uchomoaji chomoaji. Kontena nzima inapotea, vifaa vya ndani ya magari vinapotea. Hili ni jambo la kuangalia. Linawapa shida sana Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema, wenzangu wamezungumzia sana kuhusu chama, kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kuwa mgombea na kumpongeza Dr. Bilal kuwa mgombea mwenza. Nadhani hili halina ubishi la kumpongeza Dr. Shein kuwa mgombea wa Urais wa Zanzibar. Nadhani hili halina ubifishi. Watani zangu hapa wamesema sema hapa kwamba safari ijayo wanategemea watachukua madaraka. Hilo haliwezekani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeng’atuka Ubunge, lakini nitabakia kuwa mwanachama wa Chama cha Mapinduzi. Sababu ya kung’atuka, mimi sasa sio somo tena, ni nyakanga. Nyakanga kazi yake ni kuchezesha unyago, hachezeshwi. Nataka kusema kwamba mwaka 2010 mhakikishe kwamba CCM itashinda kwa kishindo, itashinda kwa kishindo Zanzibar, wala hatutazami kwa sababu Shein katoka Pemba, tunachagua Chama. Chama kwanza, mtu baadaye. Tutashinda kwa kishindo Tanzania Bara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wameshapiga kura za maoni, katika wagombea 19, saba ndio waliopata kura. Hiyo ndiyo indiketa. Hakuna sababu, kama ni pweza katabiri keshatabiri kwamba Chama cha Mapinduzi kitashinda kwa kishindo, tunaona indiketa. Sasa ndugu zangu niseme tu kwamba Chama cha Mapinduzi mwaka 2010 kitashinda kwa kishindo, na wale ambao wanapenda kuwahi hili gari nafasi bado ipo, waje tunawakaribisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kueleza hayo, nirudie tu kuwashukuru sana kama nilivyosema, mimi nimesimama hapa kwa kutangaza nia ya kutokugombea. Jimboni kwangu nimeshaaga, mpaka ninaondoka kulikuwa na vijana 24 wanataka Ubunge. Nadhani mmoja anaweza akachaguliwa akaja Bungeni. Sasa baada ya hapo, nirudie kusema naunga mkono hoja na sio mimi tu, Mheshimiwa Naibu Waziri naye nimpongeze, maana Naibu Waziri pamoja na kwamba kafanya kazi miaka mitano, lakini na yeye ameshatangaza nia ya kutokugombea. Ameamua kwenda kuchukua Ph.D kwanza, akirudi huko sasa ndiyo anarudi kwa kishindo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nakutakia kila la kheri na fanaka. Niwashukuru watumishi wote wa Bunge, niwaombe radhi wale ambao pengine niliwakwaza hapa na pale, tusameheane. Sina mtu ambaye amenikosea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kueleza hayo, nakushukuru. Ahsante sana. |
|
Records 1 to 1 of 4 |
|
|
|
|
|